'Utalii wa Kenya umekomaa kushinda Tanzania'

Safari katika mbunga ya Serengeti nchini Tanzania
Image caption Safari katika mbuga ya Serengeti nchini Tanzania

Shirikisho la Utalii nchini Kenya KTF limepinga madai kwamba Kenya imekuwa ikipoteza watalii kwa taifa la Tanzania na badala yake ikasema kuwa hakuna ushindani wowote kati ya mataifa hayo jirani.

Mwenyekiti wa bodi hiyo Mohammed Hersi amesema kuwa Tanzania ni taifa ambalo limeanza kujiimarisha kitalii huku Kenya likiwa taifa ambalo tayari limekomaa katika sekta hiyo.

Matamshi yake yanajiri wiki moja tu baada ya waziri wa utalii nchini Kenya Najib Balala kusema kuwa Kenya imekuwa ikipoteza watalii wake kwa jirani yake Tanzania kutokana na hoteli zake zilizochakaa.

''Sababu ambayo Tanzania ilifanya vyema katika sekta ya utalii zaidi ya Kenya ni kwamba hoteli zao ni mpya na za kisasa huku zetu zikiwa na miaka 40'', alisema Bw Balala.

Kulingana na waziri huyo Utalii uliipatia Tanzania $2.3 bilioni (Sh5 trilioni) mwaka uliopita kutoka $2 bilioni (Sh4.4 trilioni) 2016. Mapato hayo yalikuwa $1.9 bilioni 2015 (Sh4.18 trilioni).

Hata hivyo akizungumza na BBC Hersi alisema kuwa Tanzania ni taifa linaloshirikiana pakubwa kibiashara na Kenya hivyo basi ukuaji wowote katika sekta hiyo pia unaisaidia Kenya.

''Hatuwezi kusema kwamba Kenya imekuwa ikipoteza watalii ama kudai kwamba tunashindana na Tanzania, kilichopo ni kwamba mataifa haya mawili yanasaidiana kwa kuwa asilimia 45 ya watalii wanaoingia nchini Tanzania wanapitia nchini Kenya''.

Huwezi kusikiliza tena
'Utalii wa Kenya umekomaa kuliko wa Tanzania'

Hersi ambaye pia ni afisa mkuu mtendaji wa hoteli za Sun Africa nchini Kenya amesema kwamba Utalii wa Kenya umekomaa zaidi ya ule wa jirani yake ambao alisema kuwa unaendelea kukuwa.

''Taifa la Tanzania limekuwa kivutio kizuri cha watalii ikilinganishwa na Kenya kutokana na ile dhana kwamba kuna usalama mbali na kuwa na watu wakarimu ikilinganishwa na Kenya ambapo tulikuwa na marudio ya uchaguzi yalioathiri safari za wageni'', alisema.

"Kumbuka Kenya ni jirani ya Somalia, Kenya ina wanajeshi wake Somalia hivyo basi wale magaidi wamekuwa kila mara wakijaribu kushambulia taifa hili na watalii hawapendelei kusikia mambo kama haya. Unapokwenda Ulaya na kuanza kuinadi Kenya katika sekta ya utalii unachoulizwa ni 'je kuna usalama?", aliongezea.

Afisa huyo aidha amepinga matamshi ya Bw Balala kwamba hoteli nyingi nchini Kenya zimezeeka akisema kuwa wamiliki wa hoteli hizo wamewekeza fedha nyingi ili kuziimarisha na kuongezea kuwa zaidi ya hoteli 25 zimejengwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita jijini Nairobi pekee.

Alitaja hoteli kama vile English Point Marina mjini Mombasa iliyojengwa kwa gharama ya $50m, mbali na hoteli ya Marriot ilio na vyumba 3000.

Amesema kuwa sekta ya utalii nchini Kenya inahitaji zaidi ya bilioni 3 ili kuimarishwa kupitia kuinadi katika mataifa ya kigeni.

Haki miliki ya picha AFP

Amesema kuwa watalii wanaozuru kwa wingi taifa hilo ni kutoka Marekani-220,000, Uingereza-180,000, Ujerumani, Italia, Ufaransa na Uhispania. Wengine ni China na India.

Katika mahojiano yake ya awali katika runinga ya Citizen nchini Kenya Waziri Balala alinukuliwa akisema kuwa licha ya idadi ya watalii wanaowasili Kenya kuongezeka kutoka 1,342,899 mwaka 2016 hadi 1,474,671 mwaka 2017, Kenya ina uwezo wa kuwavutia watalii zaidi ikiwa hoteli na huduma kwa wateja zitaboreshwa.

"Changamoto kubwa tuliyo nayo sasa ni usalama. Mpaka wetu na Somalia pia unaleta wasiwasi na hofu kwa wageni wetu," alisema Bw Balala.

Kulingana na wizara ya utalii na mali asili watalii 1,137,182 waliingia nchini Tanzania mwaka 2015 na idadi hiyo ikapanda hadi watalii 1,284,279 mwaka 2016.

Utalii uliiletea Tanzania dola bilioni 2.3 mwaka uliopita kutoka dola bilioni 2 mwaka 2016. Mapato ya mwaka 2015 yalikuwa ni dola bilioni 1.9.

Je ni kweli kwamba Kenya inapoteza watalii wake kwa Tanzania?

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii