Marekani yaiwekea Korea Kaskazini vikwazo 'vizito' zaidi

Rais Donald Trump wa Marekani

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Rais Donald Trump wa Marekani

Waziri wa fedha nchini Marekani ameyaonya mataifa yanayoshirikiana kibiashara na Korea Kaskazini kwamba yanafanya hivyo yakijihatarisha yenyewe.

Akitangaza vikwazo vipya Steve Mnuchin amesema kuwa kampuni yoyote iliosaidia kufadhili mpango wa kinyuklia wa Pyeonyang itapoteza haki ya kufanya biashara na Marekani.

Pia aliambia maripota kwamba Marekani sasa huenda ikaanza kupanda na kuchunguza meli zinazo safirisha mizigo Korea Kaskazini.

Vikwazo hivyo vinalenga mabenki na kampuni zinazomiliki meli ambazo Marekani inasema zinafanya biashara na Korea Kaskazini.

Rais Trump alivitaa vikwazo hivyo vizito zaidi, lakini waandishi wanasema kuwa vikwazo kama hhivyo vilivyowekwa hapo awali vililenga mitandao ya kibiashara ya Korea Kaskziniu.

Vikwazo hivyo vinalenga zaidi ya meli 50, kampuni za uchukuzi nchini Korea Kaskazini lakini pia China na Taiwan.

Korea Kaskazini inakabiliwa na vikwazo vya kimataifa pamoja na vile vya Marekani kuhusu mpango wake wa Kinyuklia.

Lakini taifa hilo liliendeleza majaribio ya makombora yake mwaka uliopita ikiwemo majaribio ya silaha za kinyuklia mbali na kombora la masafa marefu linaloweza kufika Marekani.

Marekani inasema kuwa vikwazo hivyo vipya vinalenga kuifinya zaidi Korea Kaskazini ,kupitia kukata vyanzo vyake vya fedha na mafuta ili kutoendeleza mpango wake wa Kinyuklia.

Maelezo ya picha,

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong un

Idara ya fedha nchini Marekani imeorodhesha kampuni 16 hususan za meli zilizopo nchini Korea Kaskazini , lakini tano zimesajiliwa Hong Kong, mbili nchini China mbili Taiwan moja Panama na nyengine moja Singapore.

Meli 28 zimeorodheshwa katika orodha hiyo nyingi zikitoka Korea Kaskazini lakini mbili zina bendera ya Panama moja kutoka Comoros na moja ilio na bendera ya Tanzania.

Akizungumza katika mkutano na vyombo vya habari siku ya Ijumaa, Trump alionya dhidi ya hatua kali iwapo vikwazo hivyo havitazaa matunda.

''Iwapo vikwazo hivyo havitafanya kazi tutaingia katika awamu ya pili na awamu ya pili kitakuwa kitu kibaya pengine kibaya sana kwa ulimwengu''.

''Ni taifa taifa lisiloaminika na lisilofuata kanuni, iwapo tutakubaliana itakuwa kitu kizuri na iwapo haitawezekana , kitu kitafanyika''.

Hatahivyo hakuelezewa zaidi ni hatua ghani zitakazochukuliwa katika awamu ya pili.

Marekani imekuwa ikiuwekea utawala wa taifa hilo vikwazo tangu 2008 na vikwaza hivi vipya vinaweza kufuata vikwazo vyengine vilivyowekwa mwezi Novemba vilivyolenga meli za Korea Kaskazini pamoja na kampuni za China zinazofanya biashara na Pyongyang.

Umoja wa mataifa ulifuata nyayo hizo baada ya kuwekewa vikwazo vyengine vilivyoungwa mkono na mataifa 15 wanachama wa baraza la usalama la umoja ikiwemo hatua za kukatiza uagizaji wa mafuta kuingia Korea Kaskazini kwa silimia 90.