China kuongeza muhula wa Rais Xi Jinping baada ya mwaka 2023

Chinese President Xi Jinping pictured in 2018

Chanzo cha picha, EPA

Maelezo ya picha,

Kumekuwa na uvumi kuwa Bw Xi ataongeza muhula wake hadi kupita mwaka 2023.

Chama kinachotawala nchini China kimependekeza kuondoa sehemu katika katiba ambayo inaweka muhula wa rais kuwa mihula miwili ya miaka mitano kila muhula.

Hatua hiyo itaruhusu rais wa sasa Xi Jinping kubaki kiongozi baada ya muhula wake kukamilika.

Kumekuwa na uvumi kuwa Bw Xi ataongeza muhula wake hadi kupita mwaka 2023.

Kamati kuu wa chama mwaka uliopita iliboresha nguvu za Xi na kumfanya kuwa kiongozi mwenye nguvu zaidi tangu uongozi wa Rais Mao Zedong.

Fikra zake pia zilijumuishwa katika katiba ya chama, na kwenda kinyume na ratiba hakuna mrithi aliyetangazwa.

Kamati kuu ya chama cha kikomunisti ilipendekeza kuondoa sehemu inayosema kuwa Rais na Makamu wa Rais wa China wanastahili kuhudumu kipindi kisichozidi mihula miwili kulingana na katiba.

Kamati hiyo haikutoa taarifa za kina lakini taarifa kamili zinatarajiwa kutolewa.

Hatua hiyo inajiri wakati maafisa ya vyeo vya juu ambao wako katika kamati kuu wanatarajiwa kukutana siku ya Jumatatu mjini Beijing.

Bw Xi amekuwa madarakani tangu mwaka 2013 na chini ya mfumo wa sasa alistahili kuondoka madarakani mwaka 2023.