Mahakama yaagiza mwanasiasa Miguna Miguna aliyetimuliwa Kenya aruhusiwe kurejea

Bw Miguna Miguna (kwanza kushoto) wakati Bw Odinga alipokuwa anakula kiapo kuwa Rais wa Wananchi

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

Maelezo ya picha,

Bw Miguna Miguna (kwanza kushoto) wakati Bw Odinga alipokuwa anakula kiapo kuwa Rais wa Wananchi

Mahakama Kuu nchini Kenya imeiamuru serikali kufanikisha kurejea tena kwa wakili wa upinzani aliyefurushwa kutoka nchini humo mapema mwezi huu.

Jaji Chacha Mwita ameiagiza serikali kumpa Bw Miguna Miguna hati za kusafiria za kumuwezesha kurejea Kenya na kuhakikisha anasalia nchini humo hadi kesi yake dhidi ya serikali ikamilishe kusikizwa.

Bw Miguna, ambaye alikuwa mshauri wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga alipokuwa waziri mkuu wa nchi hiyo, aliondolewa nchini humo na kupelekwa Canada baada ya kuzuiliwa kwa siku kadha.

Bw Miguna ambaye ni mzaliwa wa Kenya alikuwa na uraia wa nchi mbili.

Serikali ilisema chini ya katiba ya zamani, Wakenya hawakuruhusiwa kuwa na uraia wa nchi mbili.

Maafisa wa serikali walisema hii ilikuwa na maana kwamba Bw Miguna alipoteza uraia wake alipochukua uraia wa Canada na kupata paspoti ya taifa hilo mwaka 1998, na kwamba alifaa kuwasilisha upya ombi la kukubaliwa kuwa raia wa Kenya baada ya katiba ya sasa kuidhinishwa mwaka 2010.

Chini ya Kifungu 17 cha Katiba ya Kenya, mtu aliyezaliwa Kenya anaweza tu kupokonywa uraia wake iwapo tu itabainika kwamba alijipatia hati ya uraia kwa njia ya ulaghai, iwapo yeye au wazazi wake walikuwa raia wa nchi nyingine, au iwapo alikuwa na umri wa zaidi ya miaka minane alipopatikana akiishi Kenya.

Kabla yake kuondolewa Kenya kwa nguvu mnamo 6 Februari, serikali ilikuwa imekataa maagizo ya kumuwasilisha Bw Miguna mahakamani mara kadha.

Wakati wa kutimuliwa kwake, alipokonywa paspoti yake ya Kenya hali iliyopunguza uwezekano wake wa kurejea Kenya kama Mkenya.

Chanzo cha picha, Andrew Renneisen

Maelezo ya picha,

Bw Miguna aliidhinisha hati ya kiapo cha Bw Odinga

Mawakili wake walipoiomba mahakama iamuru arejeshewe paspoti yake, na mahakama ikatoa agizo paspoti hiyo iwasilishwe kortini, maafisa wa serikali waliwasilisha paspoti yake kortini ikiwa imetobolewa mashimo.

Walisema hilo huwa kawaida kwa watu wanapopokonywa paspoti zao.

Bw Miguna amedokeza nia yake ya kutaka kurejea Kenya mnamo 26 Machi, siku ambayo amesema itakuwa "ya kukumbukwa katika historia yetu ya vita vya ukombozi."

Bw Miguna alikamatwa na polisi kwa mchango wake katika kuapishwa kwa Bw Odinga kuwa "rais wa wananchi", hafla iliyofanyika uwanja wa Uhuru Park, Nairobi mnamo 30 Januari.

Bw Miguna, ambaye pia ni wakili, ndiye aliyetia saini hati ya kiapo ya Bw Odinga.

Serikali ilikuwa imeeleza hatua hiyo ya kiongozi huyo wa upinzani kuwa uhaini wa hali ya juu.

Bw Odinga anadai kwamba alimshinda Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu wa 8 Agosti ambao matokeo yake yalifutiliwa mbali na Mahakama ya Juu kwa sababu ya kutokea kwa kasoro nyingi.

Mahakama iliamuru uchaguzi mpya ufanyike lakini Bw Odinga akasusia uchaguzi huo mnamo 26 Oktoba.