CUF: Serikali ya Tanzania imezidi katika kukandamiza demokrasia

Bw Mtatiro akiwahutubia wanahabari Dar es Salaam
Maelezo ya picha,

Bw Mtatiro akiwahutubia wanahabari Dar es Salaam

Chama cha Wananchi CUF nchini Tanzania kimeishutumu serikali ya Rais John Magufuli na kusema imekuwa kama kinara wa ukandamizaji wa demokrasia na siasa za vyama vingi.

Katika tarifa ya chama hicho iliyowasilishwa kwa waandishi wa habari na Mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya chama hicho Julius Mtatiro, CUF wamesema tangu kuingia madarakani serikali ya awamu ya tano imepiga marufuku shughuli za kisiasa jambo ambalo ni kinyume na ibara ya 20 ya katiba ya Tanzania

Chama hicho pia kimeeleza vitendo vya utekaji na mauaji ya viongozi wa upinzani kama miongoni mwa matukio yanayoendelea kuzorotesha hali ya demokrasia na kuweka usalama wa taifa katika njia panda.

Bw Mtatiro ameitaka serikali kulirejesha taifa la Tanzania kwenye msingi wa demokrasia.

Mtatiro amewataka vingozi wastaafu wakiwemo maraisi wa awamu zilizopita kuwashauri vingozi wa serikali ya awamu ya tano namna bora ya kulirejesha taifa katika njia sahihi.

Hayo yakijiri, kamanda wa jeshi la Polisi kanda maalumu ya Dar es salaam Lazaro Mambosasa ametangaza kuwashikilia watuhumiwa wawili wanaohusishwa na mauaji ya kiongozi wa Chadema Daniel John.

Mwanasiasa huyo alitekwa na kuuawa majuma mawili yaliyopita na mwili wake kutupwa na watu wasiojulikana katika fukwe za coco jijini Dar es salaam.

Visa vya mauaji ya kutoweka kwa watu Tanzania

  • Mauaji ya Kibiti mwaka 2017: Viongozi wa CCM, askari zaidi ya 10 na wananchi karibu 40 katika eneo la Kibiti walishambuliwa na kuuawa na watu wasiojulikana.
  • 11 Februari, 2018 Kiongozi wa Chadema Daniel John alitekwa na kisha aliuwawa kikatili wakati wa Kampeni za Uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni. Mwili wake ulipatikana mnamo 14 Februari.
  • Mnamo 7 Septemba, 2017, Mnadhimu Mkuu wa upinzani bungeni, mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu alipigwa risasi na watu wasiojulikana katika eneo la Area D Mkoani Dodoma. Bw Lissu pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika.
  • 21 Novemba, 2017 Mwandishi wa habari wa Mwananchi Communications Limited Azory Gwanda alipotea katika mazingira ya kutatanisha na mpaka sasa hajapatikana.
  • Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema Ben Saanane alipotea katika mazingira ya kutatanisha.