Mapigano yasitishwa kwa muda Syria

Ramani inayoonesha maeneo ya waasi Syria

Chanzo cha picha, Atlas

Maelezo ya picha,

Ramani inayoonesha maeneo ya waasi Syria

Rais wa Urusi Vladmir Putin ameagiza usitishwaji wa mapigano kwa takriban saa tano katika mashambulizi yanayofanywa na serikali ya Syria katika maeneo ya mashariki mwa eneo la Ghouta linalodhibitiwa na waasi.

Usitishwaji huo wa mapigano unaanza leo Jumanne na utajumuisha kuundwa kwa kile kinachoitwa '' Njia ya Hisani'' kuwawezesha raia kuondoka katika eneo hilo lenye mapigano makali.

Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu alitoa tangazo juu ya kusitishwa huko kwa mapigano, kwa kusema kuwa lityaanza kati ya saa tatu mpaka saa nane kwa saa za eneo la tukio ama saa moja mpaka saa sita GMT, kila siku.

Taarifa zaidi iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema Shirika la Msalaba mwekundu la Syria litasaidia mpango huo wa uokozi na kwamba watu watapewa taarifa kupitia vipeperushi, ujumbe wa simu na video.

Waasi wanaopiagana, wamezingirwa karibu na mji mkuu wa Damascus, ambako raia laki tatu na 93,000, wamekwama, huku mashambulizi makali yakifanywa na majeshi ya serikali yanayoungwa mkono na Urusi.

Kwa mujibu ya makundi ya waangalizi, Zaidi ya watu 560 wameuawa katika siku nane za mapambano.