Akamatwa baada ya kutekeleza mauaji katika Facebook live

Prentis Robinson alifariki akijichukua kanda ya video ya moja kwa moja ya facebook Live

Chanzo cha picha, FACEBOOK

Maelezo ya picha,

Prentis Robinson alifariki akijichukua kanda ya video ya moja kwa moja ya facebook Live

Maafisa wa polisi kaskazini mwa Carolina wanasema kuwa mtu mmoja alipigwa risasi hadi kufa alipokuwa akijichukua kanda ya video ya moja kwa moja katika mtandao wa facebook Live.

Prentis mwenye umri wa miaka 55 alikuwa ameondoka katika kituo cha polisi ambapo alikuwa ameripoti simu yake kuibwa na alikuwa akijichukua kanda hiyo kwa kutumia kijiti cha kupiga selfie.

Baadaye mtu mmoja anaonekana akirushiana naye maneno .Uko moja kwa moja katika facebook Live , Bwana Robinson anamwambia kabla ya milio ya minne ya risasi kusikika.

Mtu huyo ambaye maafisa wa polisi wanasema alikuwa amejihami na bunduki baadaye anaonekana akipita mbele ya simu hiyo huku akitoroka.

Mshambuliaji huyo aliyetajwa na maafisa wa polisi kwa jina Douglas Colson amekamatwa.

Idara ya Polisi ya Wingate ilisema kuwa bwana Colson alihojiwa siku ya Jumatatu lakini hakukamatwa wakati huo.

Siku ya Jumanne alfajiri alijiwasilisha mwenyewe katika kituo cha polisi baada ya kutoa agizo la kumkamata.

Ufyatuliaji huo wa risasi uliotokea siku ya Jumatatu ulisababisha kufungwa kwa chuo kikuu cha Wingate kilichopo kilomita 48 kusini mashariki mwa Charlotte, Carolina kaskazini.

Maafisa wa polisi wanasema kuwa bwana Robinson amekuwa akipigwa picha za facebook live ili kufichua matatizo katika maeneo jirani.

Alionekana katika kanda ya video siku ya Jumatatu akilalamika kwamba mmoja wa nduguze alikuwa amemuibia simu yake ya rununu.

Afisa mkuu wa polisi katika kituo cha polisi cha Wingate Donnie Gay alishindwa kuzungumza baada ya shambulio hilo.

Aliambia runinga ya WSOC-TV kwamba alikuwa amewasili katika kituo hicho kuripoti uhalifu.

Chanzo cha picha, CBS

Maelezo ya picha,

Douglas Colson alikamatwa na maafisa wa polisi

Inadaiwa kwamba jamaa huyo aliishi maisha yake ya utu uzima katika eneo la Wingate na alikuwa amefuzu katika shule ya upili.

Msemaji wa facebook aliambia chombo cha CBS News kwamba kampuni hiyo iliondoa kanda ya video asilia.

''Kwa sababu hatungejua kwamba mwathiriwa angetaka kitendo chake cha uhalifu kurekodiwa katika mtandao wa kijamii, tumeondoa kanda hiyo ya video'', alisema msemaji huyo.