Changamoto katika kutekeleza marufuku ya mifuko ya plastiki Kenya

Maafisa wa usalama wamekuwa wakifanya misako kuwatafuta wanaoendelea kutumia mifuko ya plastiki
Maelezo ya picha,

Maafisa wa usalama wamekuwa wakifanya misako kuwatafuta wanaoendelea kutumia mifuko ya plastiki

Uamuzi wa Kenya wa kupiga marufuku utengenezaji, ununuzi na utumiaji wa mifuko ya plastiki mwaka jana ulisifiwa sana kote duniani, na kuonekana kama njia mwafaka ya kupunguza uchafuzi wa mazingira utokanao na mifuko hii.

Miezi sita baadaye, je, kumekuwa na manufaa yoyote?

Asubuhi katika soko la City Market katikati mwa jiji la Nairobi, maafisa wa Mamlaka ya Taifa ya Usimamizi wa Mazingira (Nema) wamefika kuwatafuta wale walio na mifuko ya plastiki.

Mwuzaji mmoja anapowaona maafisa hawa anachomoka mbio kutoka kibanda chake na kuyagonga maembe yaliyokuwa yamepangwa vizuri, anatoroka kuelekea nje ya soko akihofia kukamatwa.

Katika kujinusuru anaacha kibanda chake bila muhudumu.

Maelezo ya picha,

Mifuko ya plastiki imelaumiwa kwa kuchangia uchafuzi wa mazingira

Katika kibanda hiki, karoti, pilipili, vitunguu saumu, tangawizi na bidhaa nyingine, zote zimefungwa kwa mifuko ya plastiki, vinamgoja mnunuzi tu!

Miezi sita iliyopita marufuku ya kutengeneza, kuuza au kutumia mifuko ya plastiki ilianza kutekelezwa nchini Kenya.

Viwanda vilivyokuwa vinatengeneza mifuko hiyo vingi vilifungwa au kulazimika kuanza kutengeneza bidhaa nyingine.

Mifuko kutoka Uganda

Lakini bado kuna watu ambao wanaendeleza biashara hii ya mifuko ya plastiki.

Bi Njoki Mukiri, Mkurugenzi wa Masuala ya Mazingira katika jiji la Nairobi anasema kuna watu wanaouza mifuko hii hasa katika masoko.

"Tuna taarifa kwamba mifuko hii inaagizwa kutoka nje ya nchi, hasa zaidi Uganda, Tanzania na Somalia . Tunajaribu kufuata vidokezo."

"Kwanza kabisa baadhi ya mifuko hiyo tunayoikuta ikiwa imefungiwa mboga imepigwa chapa kwamba imetoka Uganda. Tunajaribu kutumia mbinu nyingi ili kuhakikisha kwamba mifuko hii haiingizwi nchini".

Maelezo ya picha,

Wakenya wamekuwa wakitumia mifuko mbadala kubebea bidhaa

Wafanyabiashara ambao bado walikuwa na mifuko ya plastiki ambayo haijatumiwa baada ya marufuku hiyo kuanza walishauriwa kulifahamisha shirika la NEMA kuhusu hazina waliyokuwa nayo ya mifuko hiyo lakini baadhi yao hawakufanya hivyo.

Wakenya wengi tayari wametafuta njia mbadala ya kusafirisha mizigo yao.

Wanatumia mifuko isiyokuwa ya plastiki.

Kellen Kiganane anaishi Nairobi pamoja na familia yake, kwake mifukoya kutumia mara kwa mara haikosi nyumbani.

Kellen ana watoto watatu na pia ameajiriwa.

Kila wikendi yeye hupika chakula ambacho familia yake itatumia wiki nzima na kuiweka kwenye jokovu au Friji. Awali alikuwa anatumia mifuko ya plastiki kuhifadhi vyakula hivyo lakini siku hizi anatumia mikebe ya plastiki.

Rwanda, Mauritania na Eritrea ni baadhi ya nchi za Afrika ambazo zimepiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki, lakini sheria hii nchini Kenya inaonekana kuwa yenye adhabu kali zaidi ikilinganishwa na mataifa hayo.

Faini ya dola za Kimarekani 500 au kifungo cha mwaka mmoja gerezani ndiyo adhabu kwa yeyote atakayepatikana na mifuko hiyo.

Watu 150 kukamatwa

Na wale wanaotengeneza mifuko hiyo ya plastiki watatozwa faini kati ya dola elfu 20 na dola elfu 40. Tangu marufuku hiyo ianze takriban watu 150 - wamekamatwa.

Wiki iliopita, watu 29 walitozwa faini hiyo ya dola 50. Sam Barrat ni Mkuu wa Ushauri wa shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira- UNEP mjini Nairobi: „Eneo lote la Afrika Mashariki linapaswa kuchukua msimamo mmoja katika suala hili. Ikiwa kuna marufuku nchini Kenya na hakuna marufuku Uganda kuna uwezekano wa mifuko hiyo ya plastiki kupenyezwa huku."

"Lakini kile ambacho tumeshuhudia katika mikezi sita iliyopita ni mafanikio makubwa ambayo Kenya inapaswa kujivunia.

"Wameongoza vizuri sana katika hili na kujijengea sifa ulimwenguni kwa kujali na kushughulikia mazingira na imeanzisha gumzo ya mambo gani zaidi pia yanapaswa kufanywa, mfano kuhusu chupa za plastiki."

Kabla ya marufuku hii, awali Kenya ilijaribu mara mbili kupunguza matumizi ya mifuko ya plastiki bila mafanikio yoyote.

Wanamazingira wanatumai kuwa hatua hizi za awali, licha ya kukumbwa na changamoto kadha wa kadha zitachangia pakubwa katika kupunguza uchafuzi wa mazingira nchini Kenya na pengine kote duniani.