Serikali ya Rwanda yafungia zaidi ya makanisa 700

Rwandan president Paul Kagame gestures during a press conference following a high-level meeting a the International Telecommunication Union (ITU) headquarter on November 12, 2008 in Geneva.

Chanzo cha picha, AFP

Serikali ya Rwanda imeyafunga makanisa zaidi ya 700 katika mji mkuu wa nchi hiyo Kigali kwa kukosa kutimiza masharti yaliyowekwa ya usafi na usalama.

Gazeti la kibinafsi la The New Times linasema operesheni hiyo ilianza wiki moja iliyopita.

Kufikia sasa, makanisa 714 yamefungwa, pamoja na msikiti mmoja.

Afisa wa serikali Justus Kangwagye ameambia gazeti hilo la mtandaoni kwamba makanisa hayo yamekiuka sharia za usalama.

"Shughuli ya kuabudu inafaa kufanywa kwa utaratibu na kwa kutimiza masharti ya viwango vya ubora na usalama vilivyowekwa. Kutumia uhuru wako wa kuabudu hakufai kuingilia haki za watu wengine. Wametakiwa kusitisha shughuli zote hadi watimize masharti yaliyowekwa," amesema.

Amesema baadhi ya makanisa haya yalikuwa yakifanya kazi bila kuwasilisha upya maombi ya leseni na kwamba maafisa wa serikali hawataruhusu makanisa hayo yafunguliwe.

Taarifa zinasema baadhi ya makanisa yamekuwa yakifanya kazi kwa kutumia mahema na hayana maeneo ya kutosha ya kuegesha magari ya waumini.

Baadhi ya waumini wamekuwa wakiegesha magari yao pambizoni mwa barabara na kusababisha misongamano ya magari.

Wakazi wa Kigali, kwa mujibu wa gazeti hilo, wana hisia mseto kuhusu hatua hiyo.

Baadhi wanaiunga mkono lakini wengine wangependa wenye makanisa hayo wamepewe muda zaidi wa kutimiza masharti hayo.

Askofu Innocent Nzeyimana, rais wa Baraza la Makanisa katika wilaya ya Nyarugenge ameiomba serikali, kwa niaba ya makanisa, kuyaruhusu makanisa yaliyofungwa yaendelee kuhudumu yanapoendelea kufanya juhudi za kutimiza masharti yaliyowekwa.