Nduli kutoka Mashariki: Baridi kali yawaua watu 10 Ulaya

A person pulls at a snow covered branch after a heavy snowfall in Casaglia, Mugello, Florence's province, Italy, 27 February 2018. Haki miliki ya picha EPA
Image caption Theluji katika mji wa Casaglia, Italia Jumanne

Baridi kali barani Ulaya, ambayo imesababishwa na wimbi la baridi kutoka maeneo ya Siberia, Urusi, imesababisha vifo vya watu 10.

Upepo mkali wa baridi, ambao umepewa jina 'Nduli kutoka Mashariki' nchini Uingereza, unavuma kote barani, na viwango vya joto vimeshuka hadi nyuzi -30C (-22F) katika baadhi ya maeneo.

Watu 10 walikuwa wamefariki kufikia Jumatatu, na wengi wanakabiliwa na wakati mgumu kulala mijini kutokana na baridi.

Makundi ya kutoa misaada yamefungua vituo vya kutoa makao na chakula moto kwa maelfu ya watu walioathirika.

Hali ya sasa ya baridi ambayo imepewa jina 'Dubu wa Siberia' na Waholanzi na 'Makombora ya Theluji' na raia wa Sweden, imesababisha theluji kutokea katika baadhi ya maeneo ya Uhispania na Italia ambayo kwa miaka mingi hayajashuhudia theluji pamoja na visiwa vya Bahari ya Mediterranean vya Corsica na Capri.

Barabara nyingi zimefungwa, safari za treni kusitishwa na safari nyingi za ndege pia kuahirishwa katika maeneo mengi barani.

Shule nyingi pia zimefungwa na baadhi ya mashirika yamewashauri wafanyakazi wake kusalia manyumbani.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wawili hawa walipigwa picha kwenye theluji katika uwanja wa St Mark mjini Venice mapema Jumatano
Haki miliki ya picha EPA
Image caption Jumatatu, katika eneo la kale la Coliseum, Roma theluji ilishuhudiwa kwa mara ya kwanza katika miaka mingi

Maeneo mengi yamewekwa kwenye tahadhari huku baridi kali ikitarajiwa kuendelea kushuhudiwa hadi mwisho wa wiki hii.

Vituo vya dharura vya kutoa makao vimefunguliwa na serikali katika maeneo mengi kuwahudumia watu walio bila makao.

Ubelgiji, polisi wameruhusiwa kuwazuilia watu usiku kucha iwapo watakataa kwenda kwa lazima katika vituo hivyo.

Mashirika ya Msalaba Mwekundu na Hilal Nyekundu yametoa wito kwa umma kuwajulia hali majirani zao ambao huenda wamo hatarini.

"Kubisha mlango tu kwa jirani kuhakikisha yuko sawa kunaweza kusaidia sana," mkurugenzi wa mashirika hayo Ulaya Simon Missiri amesema.

"Kunaweza kuwa tofauti kati ya uhai na mauti."

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Hata katika kisiwa cha Corsica, Ufaransa, kulionekana theluji
Haki miliki ya picha EPA
Image caption Hivi ndivyo hali ilivyo bandari ya San Sebastián eneo la Bsque, kaskazini mwa Uhispania

Watu watano walifariki Poland w na wanne wamefariki Ufaransa, akiwemo ajuza mmoja aliyepatikana amefariki katika lango la kuingia kituo cha kuwahudumia wazee ambamo alikuwa akiishi, kwa mujibu wa shirika la AFP.

Watu watatu walifariki Lithuania na wawili Romania, akiwemo ajuza wa miaka 83 aliyepatikana amefariki kwenye theluji.

Mwanamume wa miaka 47 asiye na makao alipatikana amefariki katika jiji la Milan.

AFP wanakadiria wkamba kote Ulaya, idadi ya waliofariki inaweza kufikia watu 24.

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Theluji nyingi ilianguka katika mkoa wa Florence, Italia
Haki miliki ya picha EVN

Roma, theluji ilianguka mara ya kwanza katika miaka sita.

Ujerumani, kiwango cha joto katika kilele cha mlima Zugspitze kilifikia -30C, maeneo mengi nchini humo kiwango cha kadiri cha joto kilikuwa -10C.

Mjini Paris, kiwango cha joto kilifikia -6C.

Mada zinazohusiana