Tanzania yajitenga na meli 'zinazoisaidia' Korea Kaskazini

Bw Mahiga ameomba usaidizi wa kuzifuatilia meli
Maelezo ya picha,

Bw Mahiga ameomba usaidizi wa kuzifuatilia meli

Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Augustine Mahiga amewaambia mabalozi wa nchi tano ambazo ni wajumbe wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwamba meli mbili zilizoonekana zikielekea Korea ya Kaskazini zikipeperusha bendera Tanzania tayari zilishafutiwa usajili miaka miwili iliyopita.

Bw Mahiga amewaomba mabalozi hao kutoka Marekani, Uingereza, Ufaransa Urusi na China kuisadia Tanzania kuweza kuzibaini meli zinazopeperusha bendera yake na kwenda kinyume na utaratibu wa kimataifa wa wasafirishaji wa baharini.

Mabalozi hao wameahidi mataifa yao yatachangia kuisaidia Tanzania kwa vifaa vya kisasa na mafunzo ya kuweza kufuatilia mienendo ya meli inazozipatia usajili.

Juma moja lililopita Rais wa Marekani Donald Trump alitishia kuyawekea vikwazo vya Kiuchumi Kidplomasia Kisiasa na kibiashara mataifa yote yatakayokiuka vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa na Marekani kwa Korea ya Kaskazini ikiwa ni kuweka mkwamo kwa mpango wake wa kustawisha silaha za nyuklia.

Meli hizo zilizokuwa zikipeperusha bendera ya Tanzania zilionekana kwa njia ya setilaiti, moja ikielekea Korea ya Kaskani moja kwa moja na nyingine ilinaswa ikihamisha mizigo ambayo haikutambulika kwenye meli nyingine ambayo baada ya zoezi hilo la uhamishaji ilielekea Korea ya Kaskazini baada ya kupakia mizigo hiyo.

Mwezi wa kwanza mwaka huu Tanzania ilizifutia usajili meli zote 450 zilizokuwa zinapeperusha bendera yake kwenye maji ya kimataifa ikiwa ni baada ya kupatikana kwa meli iliyokuwa imebeba shehena ya silaha na dawa za kulevya huku ikipeperusha bendera ya Tanzania.

Tangu kufutwa kwa usajili huo uchunguzi uliofanyika tayari umebaini meli 119 zimetenda makosa mbali mbali ikiwemo kupeleka bidhaa kwenye nchi zenye vikwazo, kubeba silaha na dawa za kulevya, na kubeba mafuta ya wizi