Muasi wa zamani ageuka kuwa mlezi wa yatima Burundi

yatima
Maelezo ya picha,

Bi Mariam Ndayisenga maarufu kama Mama Zulu,muasi mstaafu aliyeamua kuwalea watoto yatima

Mwanamke mmoja nchini Burundi ambaye alikuwa ni miongoni mwa wanawake wa kwanza kujiunga na makundi ya waasi mwishoni mwa miaka ya 90, kwa sasa amejiingiza katika shughuli za kuwalea watoto yatima.

Athari za vita kwa watoto ndio zilizomuhamasisha mwanamke huyu ambaye alikuwa mpiganaji wa zamani wa kundi la Waasi la CNDD/FDD kufanya kazi ya kuwalea watoto hao yatima.

Bi Mariam Ndayisenga maarufu kama Mama Zulu alikutana na Mwandishi BBC,Ramadhani Kibuga katika makazi yake yaliopo Kinama kaskazini mwa jiji la Bujumbura.

Kituo chake kina watoto zaidi ya 70 wenye rika mbalimbali wakiwemo hata watoto wachanga.

Kituo hiki kinaonekana kuwa sio cha kawaida kutokana na historia ya mmiliki wa kituo hicho kuwa mstaafu katika harakati za kijeshi.

Lakini ni nini kilichomsukuma kuanza kushughulika na kazi ya kulea yatima na kuacha shughuli za uasi.

Maelezo ya picha,

Mstaafu wa waasi asema,Athari za vita zinawakumba watoto

''Mimi ni mama wa kwanza kabisa kuchukua silaha na kwenda kupigania nchi yangu lakini matokeo yake sikuwa ninayategemea kwa kuwa yalileta athari kubwa sana haswa kwa watoto.'' Bi Marium aeleza.

Katika vita alikutana na changamoto mbalimbali lakini kulea watoto hawa inampa furaha kwake na anasema hudumu za watoto kuanzia chakula , mavazi hata matibabu imekuwa sio jambo rahisi, lakini hajavunjika moyo na watu pia wanamsaidia kwa namna moja au nyingine.

Pamoja na kukutana na changamoto kadha wa kadha hata kwenye malezi ya watoto wahitaji Maryam anasema katika maisha yake amezoea kupambana.

Maana hata wakati wa vita alipewa jina la mama Zulu kwa kuwa yeye ni mama shujaa na hata anadhani ushujaa wake unahitajika kuwalea watoto hawa zaidi.

Burundi ni miongoni mwa nchi za Afrika zilizokumbwa na vita na kujikuta watoto wengi wako barabarani wakiwa ni omba omba na mayatima.

Hivyo changamoto kubwa iliosalia ni jinsi ya kuwatunza watoto hao wahitaji na yatima nchini humo.