Rwanda yaanza kufungia makanisa 700 kwa kutotimiza masharti yaliyowekwa

Baadhi ya makanisa yamekuwa yakifanya ibada kwenye mahema
Maelezo ya picha,

Baadhi ya makanisa yamekuwa yakifanya ibada kwenye mahema

Serikali ya Rwanda imeanza kutekeleza uamuzi wa kufunga makanisa ambayo hayajatimiza kanuni za ujenzi na vigezo vingine vinavyotakiwa kwa wachungaji wa makanisa hayo.

Jumla ya makanisa 700 yamefungwa, mengi yakiwa ni makanisa madogo madogo yaliyoanzishwa hivi karibuni.

Kulingana na bodi ya taifa hilo inayohusika na uongozi, makanisa yanatakiwa kufwata taratibu za ujenzi wenye miundo msingi stahiki na shahada ya elimu ya theolojia kwa wachungaji.

Mwandishi wa BBC Yves Bucyana aliyepo Kigali anasema makanisa yasiyopungua 700 na msikiti mmoja tayari yamefungwa kutokana na kile ambacho bodi ya taifa hilo inayohusika na uongozi imetaja kuwa kushindwa kutimiza kanuni za ujenzi.

Maelezo ya picha,

Makanisa zaidi ya 700 yamefungwa

Baadhi ya makanisa yanaendeshea ibada zao kwenye mahema,huku makanisa mengi yakifanyia ibada zao kwenye nyumba za kibiashara kama baa na mighahawa; na makanisa mengi yana kelele za kupita kiasi ilhali yamejengwa katikati mwa makazi ya wananchi.

Mwandishi wa BBC mjini Kigali anasema ukaguzi wa wakuu wa serikali za mitaa bado unaendelea kutathmini makanisa zaidi yasiyotimiza masharti na pengine kufungulia mengine ambayo yamo mbioni kutimiza matakwa ya serikali.

Rwanda inajadili sheria mpya ambayo itahusu mashirika yenye misingi ya imani na dini yanayoendeshwa na wahubiri kuwa wahubiri hao lazima wawe na shahada za elimu ya theolojia.

Wakosoaji wanaona kwamba hii ni sheria inayolenga kudhibiti makanisa wakati wengine wanaona kwamba ni sheria yenye lengo la kunyoosha makanisa ambayo siku hizi yamezongwa na migogoro ya ndani.