Wanamgambo wa al-Shabab waua polisi watano kaskazini mwa Kenya

Wapiganaji wa Al- Shabaab nchini Somalia Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wapiganaji wa Al- Shabaab nchini Somalia

Polisi watano wa Kenya wameuawa na wengine watatu kujeruhiwa vibaya katika shambulio linaloaminika kutekelezwa na wanamgambo wa Kiislamu wa al-Shabaab katika eneo la Fino, katika kaunti ya Mandera kaskazini mwa nchi hiyo.

Naibu kamishena mkuu wa eneo hilo Eric Oronyi, anakisia kuwa kati ya wapiganaji 70 au 100 hivi, waliokuwa na silaha kali, walivamia kambi ya polisi mapema leo alfajiri na kuiteketeza kabisa.

Amesema kuwa maafisa wengine watatu walijeruhiwa, na mmoja wao yuko katika hali mbaya, shirika la habari la Reuters limeongeza.

Bwana Oronyi amesema kwamba washambuliaji hao waliharibu mtambo wa mawasiliano, kabla ya kuvamia kambi hiyo.

"Mnara wa mawasiliano, ambao ulikuwa ukilindwa na polisi wa akiba, ulipigwa bomu na kwa sasa, hakuna mawasiliano yoyote ya simu hata ya rununu katika eneo hilo", amesema Bw Oronyi.

Kundi hilo la wapiganaji, ambalo limekuwa likitekeleza mashambulio mara kwa mara kutokea nchi jirani ya Somalia, mara kwa mara limekuwa likiwalenga maafisa wa usalama na magari ya umma, kuvamia maskani ya watu na matimbo ya mawe na kuwauwa watu wengi kwa kuwapiga risasi.

Image caption Ramani ya Kenya

Kaunti ya Mandera, inapakana na nchi ya Somalia, jambo ambalo limewaacha wapiganaji hao kutekeleza maovu yao kwa urahisi.

Katika mwaka mmoja uliopita, kundi hilo la wapiganaji wa Kiislamu, limekiri kutekeleza mauaji ya watu kadha eneo la Mandera.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii