Magavana na wabunge wa Kenya waliopoteza viti vyao mahakamani

Majaji wa mahakama ya juu nchini Kenya
Image caption Majaji wa mahakama ya juu nchini Kenya

Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu nchini Kenya Agosti 8, 2017 na kufuatiwa na uamuzi wa mahakama ya juu nchini humo wa kufutiliwa mbali ushindi wa Uhuru Kenyatta, baadhi ya walioshindwa walipata matumaini na kuwasilisha kesi dhidi ya wapinzani wao.

Leo ilikuwa siku ya mwisho kwa mahakama kutoa uamuzi kuhusu kesi zilizowasilishwa kuhusu uchaguzi huo na kufikia sasa magavana watatu wamepoteza viti vyao na wabunge wanane.

Magavana

Martin Wambora

Katika orodha ya magavana waliopoteza viti vyao baada ya wapinzani wao kupeleka kesi katika Mahakama Kuu; wa kwanza alikuwa Bwana Martin Wambora, Gavana wa kaunti ya Embu. Na miongoni mwa makosa yaliyotajwa yalifanyika, ni ukosefu wa uwazi katika zoezi hilo. Jaji alisema kuwa fomu nambari 37A katika vituo 12 vya upigaji kura zilikosekana, huku karatasi za kupigia kura zikikosa alama maalum iliyohitajika.

Mohamed Abdi

Uchaguzi wa kiti cha Ugavana katika kaunti ya Wajir, pia umefutiliwa mbali, huku Jaji wa Mahakama ya juu Alfred Mabeya, akisema kuwa shughuli hizo hazikufuata sheria.

Pia ilibainika kuwa stakhabadhi za masomo ya Gavana Mohamed Abdihazikuwa zote, na pia ana shahada feki ya Chuo Kikuu.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Maafisa wa IEBC wakihesabu kura nchini Kenya

Cyprian Awiti

Februari 20, Gavana wa Homa Bay Cyprian Awiti, alishtuliwa mno na uamuzi wa mahakama ya juu, baada ya uteuzi wake kama gavana wa kaunti hiyo, kutupailiwa mbali.

Jaji Joseph Karanja, alisema katika uamuzi huo kuwa tume ya uchaguzi nchini Kenya (IEBC) haikuendesha uchaguzi wa huru na haki. Alitangaza marudio ya uchaguzi mwingine ufanyike katika kipindi cha siku 60 zijazo.

Haki miliki ya picha AFP/Getty
Image caption Mawakili waliokuwa wakishiriki kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 8

Wabunge

Babu Owino

Na mapema siku ya Ijumaa, mbunge wa Embakasi Mashariki, Bwana Babu Owino, amekuwa mbunge wa 6 kupoteza kiti chake, baada ya mpinzani wake Francis Mureithi, kuwasilisha kesi mahakamani.

Mahakama Kuu imesema kuwa uchaguzi wa Agosti 8, 2017, ambao Bwana Owino alitangazwa mshindi, ulikumbwa na makosa mengi na uvunjaji wa sheria.

Jaji katika kesi ya Bwana Babu Owino, ambaye zamani alikuwa kinara mkuu wa wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Nairobi, na ambaye amezuiwa korokoroni mara kadha kwa kutuhumiwa kumtukana Rais Uhuru Kenyatta, ilisikizwa na kuamuliwa na Jaji Joseph Sergon.

Chris Karan

Mbunge wa Ugenya Chris Odhiambo Karan, ni miongoni mwa wanasiasa ambao wamepoteza viti vyao baada ya mpinzani wake David Ochieng kupinga kuchaguliwa kwake katika uchaguzi mkuu uliopita.

Mahakama Kuu mjini Kisumu,chini ya Jaji Tripsisa Cherere, iliamua kesi hiyo na kusema kuwa, kampeini ya Bwana Karan ilikuwa ya "kupotosha na utovu wa maadili" na kwamba zoezi nzima ya uchaguzi mkuu huko Ugenya, ulikumbwa na udanyanyifu mwingi. Pigo lingine alilopata Bwana Karan ni kulipa Dola 70,000 kama malipo ya gharama ya kesi hiyo.

Wanjiku Kibe

Mwezi Mpya huu wa Machi 1, Mahakama Kuu mjini Kiambu, ilitupilia mbali ushindi wa Bi Wanjiku Kibe kama mbunge wa Gatundu Kaskazini.

Mahakama hiyo ilisema kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na udanganyifu mkubwa hasa ndani tume ya kusimamia uchaguzi nchini Kenya- IEBC.

Mlalamishi katika kesi hiyo, alikuwa mbunge wa zamani Clement Waibara.

Alfred Keter

Mbunge mbishani wa chama tawala cha Jubilee, ambaye anawakilisha eneo bunge la Nandi Hills katika maeneo anakotoka naibu Rais William Ruto la Bonde la Ufa, Bwana Alfred Keter, alipoteza kiti chake Alhamisi ya wiki iliyopita, baada ya Jaji wa mahakama kuu mjini Eldoret, Kanyi Kimondo, alipoamua kuwa uchaguzi huo ulikumbwa na kasoro chungu nzima. Mara baada ya uamuzi huo wa mahakama, Bwana Keter aliwahutubia wafuasi wake na akamkashifu moja kwa moja naibu Rais kwa masaibu haya yote anayopitia.

Kangogo Bowen

Mwenzake wa eneo bunge la Marakwet Mashariki, Bwana Kangogo Bowen ambao wote mara kwa mara wamekuwa wakimkashifu Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto, baada ya kuondolewa katika kamati maalum za bunge, pia alikabiliwa na kisu hicho hicho cha mahakama kuu.

Uchaguzi huo sasa utarudiwa, kwani jaji huyo huyo George Kimondo, ndiye aliyeamua ya Bwan Bowen.

Mahakama hiyo ilisema kuwa, vituo viwili vya kupigia kura, havikuwa vimeorodheshwa kwenye gazeti rasmi la serikali lakini vilitumika kusawazishia matokeo ya kura kabla ya kutumwa Nairobi.

Haki miliki ya picha AFP/Getty
Image caption Mtambo wa kuwatambua wapiga kura

Stanley Muthama

Wapigaji kura katika eneo bunge la Lamu Magharibi, watarudia tena zoezi la kupiga kura baada ya mahakama ya juu nchini Kenya kufutilia mbali uteuzi wa Stanley Muthama, mwanasiasa wa mara ya kwanza Bungeni, aliyewania kiti hicho kwa tiketi ya chama cha Maendeleo Chap Chap.

Katika uamuzi wa kesi hiyo, mahakama pia iliiamuru tume ya uchaguzi mkuu nchini humo, IEBC na afisa msimamizi wa uchaguzi, kumlipa mlalamishi Bwana Rishad Ahmed Amana, Dola 30,000 kama gharama ya kesi hiyo.

Ahmed Kolosh

Mbunge mwingine wa eneo bunge la Wajir Magharibi Ahmed Kolosh amepoteza kiti chake. Jaji Francis Tuiyott, alisema kuwa matokeo kutoka maeneo mawili ya upigaji kura, Qara na Korich, yalionyesha kuwa kura zilizopigwa huko, zilishinda idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura.

Alisema kuwa hatua hiyo ilikuwa tu makusudi na ni tendo la uhalifu. Aliamrishwa pia kumlipa mlalamishi Dola laki 1.5.

Joyce Emanikor

Mwanasiasa pekee wa kike kukabiliwa na hatua ya kufutiliwa mbali kwa uteuzi wake ni mwaakilishi wa kina mama kaunti ya Turkana Kaskazini mwa Kenya Bi Joyce Emanikor wa chama cha Jubilee.

Ghasia zilianza ndani na nje ya mahakama kuu mjini Lodwar, mara baada ya jaji Daniel Ogola kufutilia mbali uteuzi wa Bi Emanikor. Walinda usalama waliitwa kutuliza ghasia hizo na kudumisha amani.

Walionusurika

Leo wabunge wanane wamenusurika, baada ya kesi zilizowasilishwa dhidi yao kutupiliwa mbali.

Miongoni mwa walionusurika ni William Kamoti wa Rabai, Sylvanus Osoro wa Mugirango Kusini, Emmanuel Wangwe waNavakholo, Jessica Mbalu wa Kibwezi Mashariki, Julius Mawathe wa Embakasi Kusini, Ahmed Bashane Gaal wa Tarbaj, Enock Kibunguchy wa Likuyani na Mohamed Dahir Duale wa Daadab.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii