Museveni amfuta kazi mkuu wa polisi Kale Kayihura na waziri wa usalama Henry Tumukunde

Inspekta mkuu wa polisi Uganda Kale Kayihura
Image caption Inspekta mkuu wa polisi Uganda Kale Kayihura

Rais wa Uganda Yoweri Museveni, amemfuta kazi Inspekta mkuu wa polisi, Kale Kayihura na waziri wa Usalama, Henry Tumukunde.

Jenerali Kayihura, ambaye ni mkereketwa wa vita vilivyomsaidia rais Museveni kuingia madarakani mwaka 1986, kwa wakati mmoja alikisiwa kuwa afisa mwenye mamlaka makubwa zaidi katika jeshi la Uganda.

Lakini amekabiliwa na shinikizo kwa kushindwa kukabiliana na ukosefu wa usalama.

Mwandishi wa BBC aliyepo Uganda Isaac Mumena anasema makundi ya kutetea haki za binadamu nchini Uganda yamefurahia kutimuliwa kwa mkuu wa jeshi la Polisi, wakisema jeshi la polisi lilikuwa limeshindwa kulinda usalama wa raia na mali zao wakiongozwa na kinara wao Jenerali Kale Kayihura.

Zaidi ya wanawake 20 wameuawa katika visa vya mauaji ambavyo havijatatuliwa katika maenoe yanayouzunguka mji mkuu wa Kampala, na katika miezi mitatu iliyopita raia watatu wa kigeni pia wameuawa.

Naibu wake Okoth Ochola anashikilia wadhifa huo.

Haki miliki ya picha @KagutaMuseveni TWITTER

Kwa mujibu wa ujumbe alioandika rais Museveni katika mtandao wa Twitter, amesema: " Kwa uwezo wa mamlaka niliyopewa kikatiba, nimemteua Jenerali Elly Tumwiine kama waziri wa usalama. Nimemteua pia bwana Okoth Ochola kama afisa mkuu wa polisi. Niabu wake atakuwa ni Brigedia Sabiiti Muzeei.

Mnamo Mei mwaka 2017 Rais Museveni alimteua upya Kayihura kama mkuu wa polisi kwa muhula mwingine wa miaka mitatu,hadi mwaka 2020.

Uteuzi huo ulikumbwa na mzozo na haukudumu.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii