Habari za uzushi zinasambaa zaidi ya za kweli

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Taarifa za uzushi usambaa zaidi

Utafiti kuhusu taarifa za uzushi zipatazo 126,000 zilizoandikwa katika mtandao wa kijamii wa Twitter katika miaka zaidi ya 11, zimebainika kuwa ziliweza kusambaa kwa haraka na kuwafikia watu wengi zaidi ya taarifa za ukweli.

Utafiti huo ulifanywa na chuo cha tekinolojia cha Massachusetts.

Watafiti hao wanasema habari zisizo za kweli huwa zina mfanano wa kuvutia kama simulizi za hadithi ndio maana watu wengi huvutiwa kuzisikiliza au kusoma.

Utafiti umeonyesha kwamba taarifa za uongo za kisiasa ndio husambaa zaidi ya taarifa nyingine.

Na taarifa nyingine za uongo zinazosambaa zaidi ni ambazo zinahusiana na habari za miji mikubwa,biashara,ugaidi ,sayansi ,burudani na majanga ya asili.

Aidha mhadhiri wa chuo kikuu cha Edge Hill University kilichopo Lancashire, Mwanasaikolojia Geoffrey Beattie ameiambia BBC kuwa inategemea na wadhifa wa mtu anayetuma kwa wengine ambao hawajasikia taarifa hiyo kabla bila kujali kuwa ni ujumbe wa kweli au wa uongo.

''Watu wanataka kupata taarifa ambazo zinaaminika kuwa nani kasema hivyo suala la ukweli wa taarifa hiyo huwa hauangaliwi sana"

Taarifa za kizushi zisizothibitishwa huwa zinavutia hivyo watu kuhofia kuwa ni za kweli au la, huwa ni jambo la mwisho kulizingatia.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Suala la taarifa za uongo kupendwa zaidi sio katika mitandao ya kijamii peke yake bali hata kwenye maisha ya binadamu ya kila siku

Padre Maziku Leonis mwanasaikolojia kutoka chuo kikuu cha Mtakatifu Agustino nchini Tanzania anasema taarifa zisizo za kweli husambaa haraka kutokana na uvivu wa watu, kupenda kusikiliza vitu rahisi ambavyo havijafanyiwa utafiti.

Maziku anasema akili ya binadamu imegawanyika katika sehemu tatu ;kwanza binadamu wanapenda kupata taarifa ambayo inamfurahisha kwa haraka, pili binadamu anapenda kuhoji na mwisho kupata taarifa iliyo kamilifu.

Ila watu wengi uchagua kutumia sehemu ya kwanza ambayo inampa raha ya muda kwa muda mfupi kwa sababu ya uvivu wa kufikiri au kuhoji ma kutofanya utafiti.

Mwanasaikolojia huyo anaamini kuwa ulimwengu wa sasa hauwezi kwenda vizuri kama watu hawana au hawatumi elimu ya sayansi ambayo itawasaidia kutenganisha ukweli na uongo.