Je unafikiri unamfahamu Mt. Maria Magdalena?

Mary: Rooney Mara kwenye filamu Mary Magdalene Haki miliki ya picha UNIVERSAL
Image caption Mary: Rooney Mara kwenye filamu Mary Magdalene

Filamu mpya kuhusu Maria Magdalena inathibitisha mtazamo uliopo kuwa alikuwa kahaba aliyeokolewa na Kristo.

Yesu wa Nazareti, Yesu Kristo.Jaribio la mwisho la Kristo.Filamu kadhaa na hata maigizo ya jukwaani huonyesha Maria Magdalena kuwa mwanamke mwenye dhambi aliyeokolewa na mwana wa Mungu.

Filamu mpya, inamuonyesha alikuwa shuhuda wa kifo cha Yesu na ufufuko wake na ambaye anastahili kutazamwa kama mtume.

Huenda ikazua mjadala kwa watu wanaoamini madhehebu ya Orthodox kuwa Maria Magdalena alikuwa kahaba.

Hata hivyo Rooney Mara na Garth Davis, nyota na muongozaji wa filamu ya Maria Magdalena, wamejiandaa kukabili hali yoyote ya mkanganyiko itakayowakabili.

Madai kuwa Maria alikuwa mfanyabiashara wa ngono yametoka kwa Papa Gregory wa kwanza, mwaka 951, aliyemtaja kuwa kahaba aliyetubu.

Ni mtazamo ambao umeendelea kuwepo kwa karne na karne.

Haki miliki ya picha UNIVERSAL
Image caption Joaquin Phoenix ameigiza kama Yesu

Lakini hakuna uthibitisho wa kuwa Maria alikuwa kahaba au mwenye dhambi kwenye maandiko ya agano jipya. Hayo yameelezwa kuzungumziwa kwenye kitabu cha Marko na Luka, vikieleza habari ya kukemewa mapepo yatoke ndani yake.

Kuweka ushahidi wote pamoja ni rahisi kuhitimisha kuwa Maria amekuwa mhanga wa kutazamwa vibaya kwa miaka 1,400.

Kanisa Katoliki ''lilisafisha'' jina la Maria mwaka 1969, wakati Papa Francis alipomtambua kuwa ''Mtume wa Mitume''mwaka 2016.

''Kadri nilipoendelea kujifunza habari za Maria alikuwa nani hasa,ndivyo nilivyozidi kushangazwa kuwa watu wengi walimfahamu kuwa kahaba'',alisema Mara.

''Watu wote hawa walio kwenye hadithi wana makanisa duniani yakiwa na majina yao, lakini bado alijulikana kwa jina kahaba, ikanifanya nipate hasira."

''Kufahamu kuwa ulikuwa uvumbuzi wa Papa Gregory ulikuwa wa kustaajabisha na kuwa hadithi ya Maria haikuwahi kuvuma''.

Haki miliki ya picha UNIVERSAL
Image caption Sehemu ya filamu ya Mary Magdalene

''Nilifikiri kuwa habari yake ni lazima isimuliwe, na nikajisikia kuguswa zaidi kuieleza hadithi hii kumhusu,mara tu nilipojua kuwa imekuwa ikifichwa kwa muda mrefu''.

Maria tunaemuona kwenye Maria Magdalena ni mwanamama kutoka kijiji cha uvuvi Galilaya ambaye kipaji chake cha ukunga kilimfanya atengwe.

Aliposikia jina la Yesu akihubiri eneo alilokuwa akiishi,alihitaji kutiwa moyo kidogo ili kumtafuta na kuwa mfuasi wake.

Hatimaye alikuwemo kwenye karamu ya mwisho,alimshuhudia Kristo akisulubiwa na akawa mtu wa kwanza kushuhudia ufufuko wake.

''Kuna masuala mengi kumuhusu yaliyonigusa,''amesema Mara,''hakuwa na msaada,lakini alikuwa na nguvu na moyo wa kufuata anachoamini.

''Imani yake na upendo wake kwa Mungu vilikuwa muhimu sana, aliacha vyote katika maisha yake na kuamua kuyafuata hayo,nafikiri ni jambo la heri sana''.

''Maria alikuwa na upande mwingine wa wito wa kiroho'', amesema Davis.'' ''kwangu ilikuwa changamoto katika kumjenga Maria kuwa mhusika kwenye filamu.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Garth Davis (kushoto) akiwa na Harvey Weinstein kwenye tamasha la filamu la Zurich mwaka 2016

Rooney ni mmoja wa waigizaji wazuri sana na mwenye kuonesha hisia za kweli, ni wa kipekee na nilifikiri ataigiza vizuri na kwa namna ya kuvutia kuhusu maisha ya Maria.

Yesu mwenyewe nafasi yake inachezwa na Joaquin Phoenix, ambaye alishawania tuzo ya Academy mara tatu. Joaquin ni mpenzi wa Mara.

''Nililenga kumjenga Yesu kumhusisha na ubinaadam na utakatifu vyote kwa pamoja,''anasema Davis.

''Joaquin amemudu kuonyesha uhalisia kwenye uigizaji na kutupitisha kwenye mwanga na giza kwa kwa ustadi mkubwa."

Filamu ya Maria Magdalene ilikuwa itolewe nchini Marekani na Kampuni ya Weinstein.

Hata hivyo kufa kwa kampuni hiyo wakati kukiwa na shutuma za unyanyasaji wa kingono dhidi ya Harvey Weinstein, imefanya kampuni hiyo kutojulikana mustakabali wake.

Weinstein alikana shutuma hizo dhidi yake.

''Lengo langu ni kuhakikisha filamu hii inatazamwa, na itakuwa jambo baya sana kama haitatazamwa Amerika ya Kaskazini'', alisema Davis.

Filamu ya Maria Magdalena itatolewa na Kampuni ya Universal nchini Uingereza tarehe 16 mwezi Machi.