Rais wa Mauritius Gurib-Fakim amekataa kujiuzulu kufuatia kashfa ya matumizi ya fedha

Mauritian President Ameenah Gurib-Fakim Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ameenah Gurib-Fakim ni mwanamke wa kwanza Mauritius kupata urais mwaka 2015

Rais wa kike pekee barani Afrika, rais wa Mauritius, Ameenah Gurib-Fakim amekataa kuachia ngazi kufuatia kashfa ya matumizi mabaya ya fedha, siku moja baada ya kutangazwa kwamba atang'atuka madarkani.

Bi Gurib-Fakim amekanusha madai kwamba alitumia maelfu ya dola kwa matumizi binafsi kwa kutumia kadi ya benki ya shirika la msaada.

Ofisi yake imesema matumizi hayo yalikuwa bahati mbaya na fedha zimerudishwa.

Waziri mkuu wa nchi hiyo alisema angejiuzulu siku ya Jumatatu.

Lakini ofisi ya Rais imekanusha taarifa hizo.

"Mheshimiwa Ameenah Gurib-Fakim, hana hatia yoyote na ametoa ushahidi wakutosha hivyo amekataa wazo lolote la kuachia madaraka." taarifa kutoka ofisi ya rais imesema.

Taarifa hiyo imeongeza pia kwamba Gurib-Fakim, ambaye ni mwanasayansi maarufu, ' alikuwa na kadi iliyofanana kutoka benki sawa na hiyo iliyotumiwa na shirika la misaada na kwa bahati mbaya akaitumia kununua vitu binafsi'

Ofisi yake imesema dola za kimarekani 27,000 zimerudishwa na Bi Gurib-Fakim atachukua' hatua za kujitetea kisheria'

Gazeti la ndani L'Express liliripoti kuwa mwezi Februari rais wa kwanza wa kike wa nchi hiyo alitumia kadi ya benki aliyopewa na shirika la msaada la London's Planet Earth Institute (PEI) kununua vito vya thamani na nguo za gharama alipokuwa nje ya nchi.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, alipewa kadi hiyo kwa kazi yake kama mkurugenzi wa kujitolea na ilitakiwa kutumiwa kulipia matangazo ya mafunzo ya ngazi ya falsafa ya udaktari (PHD) yaliyopewa jina lake.