Upasuaji Kimakosa: Muuguzi Kenya akiri kuchanganya wagonjwa

Kenyatta National Hospital Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mwanaume aliyepasuliwa kichwa alikuwa anauvimbe wa ubongo ambao haukuhitaji upasuaji

Muuguzi katika hospitali kuu nchini Kenya amekiri kufanya kosa la kumpeleka mgonjwa asiyehitaji upasuaji katika chumba cha upasuaji.

Amesema hiyo ni kutoka na kazi nyingi alizokuwa nazo.

Mary Wahome amesema aligundua kosa lake baada ya madaktari kufanya upasuaji na kusema hawakuona uvimbe kwenye ubongo wa mgonjwa huyo.

Madaktari wa hospitali ya taifa ya Kenyatta jijini Nairobi walitakiwa kumpasua mgonjwa aliyekuwa na mgando wa damu kwenye ubongo. Lakini aliyepasuliwa hakuwa anahitaji kupasuliwa.

Kosa hilo lililozua gumzo ulimwenguni kote mapema mwezi huu lilimemuacha mgonjwa Samuel Wachir, mgonjwa aliyepasuliwa kimakosa, bila fahamu.

Bi Wahome ni mmoja wa wafanyakazi wa hospitali kuu ya Kenya ambao wamehojiwa na kamati maalum ya bunge siku ya Jumatano.

Wanakamati waliambiwa kuwa wagonjwa wenye vyumba vya pekee yao, ndio wanaopata vibandiko vya majina yao.

Kufuatia kesi hio vyombo vya habair vya ndani wamehoji uwezo wa hospitali hio kuwa na mifumo mwafaka za kuwatambua wagonjwa.

Bi Wahome amesema mchanganyiko huo ulitokea baada ya Bw Wachir kuitikia alipoita jina la mgonjwa aliyepaswa kupasuliwa, John Nderitu.

"Niliingia kwenye wadi na nikaita jina. Mtu akajibu na nikaanza kumtayatrisha mara moja,nikaandika jina lake kwenye kibandiko na kukiweka kwenye gauni alilokuwa amelivaa." alisema Bi Wahome.

Haki miliki ya picha AFP/Getty

Alikuwa miongoni wa wauguzi watatu waliokuwa wakisimamia wagonjwa 61 siku hio, kwa mujibu ya vyombo vya habari vya ndani.

Tukio hilo lilipelekea wafanyakazi wanne kufukuzwa kwa muda wakiwemo daktari wa upasuaji wa ubongo, muuguzi aliyekuwa akisimamia wadi, na afisa wa kuwatia ganzi wagonjwa.

Walirudi kazini baada ya mamia ya madaktari walipoandamana dhidi ya kufukuzwa kwa muda kwa daktari wa upasuaji wa ubongo, wakisema kuwa aliyechanganya majina ya wagonjwa ndiye aliyepaswa kwenda nyumbani.

Kisa karibu sawa Tanzania

Kwa upande wa Tanzania, kisa kama hiki kiliwahi kutokea mwaka 2007.

Tarehe 8 Novemba, madaktari wawili wa upasuaji wa ubongo katika hospitali ya rufaa ya Muhimbili walimpasua kichwa Emmanuel Didas kutoa uvimbe ambao haukuwepo.

Wakati mgonjwa Emmanuel Mgaya, aliyekuwa na uvimbe huo alipasuliwa goti.

Madaktari hao walichukuliwa hatua na kufutwa kazi na mamlaka ya hospitali.

Makosa Uingereza na India

Si Afrika pekee ambapo makosa kama hayo hufanyika. Kipindi cha BBC cha Victoria Derbyshire mwaka jana kilibaini kwamba makosa takriban 1,400 hufanyika kila wiki katika hospitali za kujifungulia kina mama nchini England kila wiki.

Mwishoni mwa mwaka jana nchini India, mtoto aliyekuwa amedaiwa kufariki baada ya kuzaliwa katika hospitali moja mji mkuu wa Delhi alibainika kuwa hai jamaa zake walipokuwa wanaelekea kumzika.

Mada zinazohusiana