Mke wa mwana wa Trump aomba talaka Marekani

Donald Trump Jr and his wife Vanessa Trump. Photo: July 2016 Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Donald Trump Jr na Vanessa Trump walifunga ndoa 2005

Mke wa Donald Trump Jr, mwana wa kiume wa kwanza wa Rais wa Marekani Donald Trump amewasilisha ombi la kutaka kumpa talaka mumewe, vyombo vya habari Marekani zimeripoti.

Taarifa zinasema Vanessa Trump anataka talaka isiyo na mvutano kwa mujibu wa ombi alilowasilisha katika mahakama moja New York.

Wawili hao, wote ambao wana miaka 40, walifunga ndoa 2005.

Wamejaliwa watoto watano.

"Baada ya miaka 12 kwenye ndoa, tumeamua kila mtu aende njia yake," wawili hao walinukuliwa wakisema kwenye jarida la habari mtandaoni la Page Sit.

"Tunaomba haki yetu ya kuishi maisha ya faragha iheshimiwe."

Wawili hao hawakutoa maelezo zaidi.

Talaka isiyo na mvutano ina maana kwamba wawili hao hawatazozana kuhusu kugawana mali yao na kuhusu nani atabaki na watoto wakati wa kusikilizwa kwa ombi lao la talaka.

Mapema mwaka huu, vyombo vya habari Marekani viliripoti kwamba wawili hao walikuwa wanakabiliwa na matatizo kwenye ndoa yao.

Walisema chanzo cha matatizo hayo ni safari za mara kwa mara za Bw Trump Jr na hatua yake ya kupenda sana kutumia mitandao ya kijamii.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Donald Trump Jr kwa sasa ni mkurugenzi mtendaji wa shirika la Trump Organization

Donald Trump Jr ni nani?

Trump Jr ndiye mwana wa kwanza wa kiume wa Donald Trump na mke wake wa kwanza Ivana Trump.

Kwa sasa ni makamu wa rais mtendaji wa shirika la The Trump Organization.

Alimuoa Vanessa Haydon baada ya wawili hao kukutanishwa katika hafla ya maonyesho ya mitindo na babake.

Safari yake ya kupata umaarufu imekabiliwa na utata kiasi.

Upendo wake, na nduguye Eric, wa kuwinda wanyama wakubwa ulikosolewa baada ya picha kutolewa zikiwaonesha wakipigwa picha na wanyama waliouawa, wakiwemo chui na mamba. Donald Jr alikuwa pia ameshika mkia wa ndovu uliokuwa umenyofolewa kutoka kwa ndovu.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii