Hezron Mogambi: Kuna dalili muungano wa upinzani Kenya unaelekea ukingoni

Bw Musyoka (kulia) na wenzake wawili wameonakana kutofautiana na Bw Odinga Haki miliki ya picha AFP/Getty
Image caption Bw Musyoka (kulia) na wenzake wawili wameonakana kutofautiana na Bw Odinga

Matukio ya hivi punde nchini Kenya yanaonyesha siasa za Kenya kuchukua kondo na mwelekeo mpya hasa baada ya mkutano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa muungano wa upinzani National Super Alliance (Nasa), Bw Raila Odinga.

Mkutano wa viongozi hawa wawili walio na uungwaji mkono wa Wakenya wengi uliwashtua wachambuzi wengi wa kisiasa nchini Kenya maana habari kuhusu kupangwa kwake na ilikuwa siri kubwa kabla ya hapo.

Lakini yaliyofuata baadaye, yametishia umoja katika muungano huo. Je, muungano huo utasambaratika? Ili kupata jibu, ni vyema kuangalia yalitokea kabla ya mkutano huo na historia ya siasa Kenya.

Kabla ya tukio la mkutano huu wa mahasimu hawa wawili wa kisiasa nchini Kenya, kiongozi wa upinzani Raila Odinga alikuwa amekataa kumtambua Rais Uhuru kama Rais wa Kenya pamoja na kuitisha uchaguzi mpya.

Itakumbukwa kuwa Kenya ilifanya uchaguzi mara mbili mwaka uliopita (mwezi wa Agosti na mwingine mwezi wa Oktoba) kulingana na agizo la Mahakama ya Juu baada ya kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa mwezi wa Agosti mwaka jana. Raila Odinga alisusia uchaguzi wa Oktoba ambapo Rais Kenyatta alichaguliwa.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na mahasimu hao wa siasa za Kenya ambao sasa wamekubaliana kufanya kazi pamoja, kazi kwao itakuwa kuleta Wakenya pamoja.

"Mkutano huu unaonyesha mwanzo mpya kwa nchi yetu, alieleza Rais Uhuru Kenyatta katika ujumbe wake baada ya mkutano akiandamana na Raila Odinga.

"Tunaweza kuwa tunatofautiana kisiasa lakini tunafaa kuwa kitu kimoja kama Wakenya kuhusiana nay ale yanakumba taifa letu."

'Ndugu wawili'

Raila Odinga alisema, "Ukweli ni kwamba tunafaa kuwaokoa watoto wetu kutokana na vitendo vyetu visivyofaa. Alimuita Rais Kenyatta, "Ndugu yangu" huku akisisitiza kwamba wawili hao walikuwa wamekuja pamoja ili kuleta Wakenya wote pomoja.

"Leo, tumekataa kuwa viongozi ambao waliiongoza Kenya katika kukosa utaifa," aliongeza.

Mkutano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga ulifanyika masaa machache tu kabla ya aliyekuwa Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Rex Tillerson kufika nchini Kenya kwa ziara ya siku tatu, ingawa washirika wa viongozi hawa wawili wa Kenya walieleza kuwa tukio hilo lilikuwa sadfa tu.

Ikumbukwe kuwa hii si mara ya kwanza kwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga kushirikiana na serikali. Katika mwaka wa 2007-2008, baada ya uchaguzi na kutokea kwa ghasia na vifo vya Wakenya zaidi ya 1,000, Raila Odinga aliweza kuungana na Mwai Kibaki kama waziri mkuu katika serikali ya muungano wa kitaifa.

Aidha, Raila Odinga amewahi kushirikiana na serikali wakati wa utawala wa rais mstaafu Daniel Moi miaka ya awali, hatua ambayo wengi wanaitazama kama mwanzo wa mwisho wa chama cha KANU.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Raila Odinga (kulia) amekuwa akikataa kumtambua Uhuru Kenyatta kama rais halali wa Kenya

Katika mkutano wa sasa, Rais Uhuru Kenyatta na bwana Raila Odinga walieleza kuwa nia ya mkutano wao lilikuwa kuratibu malengo ya viongozi hawa wawili na kupigana dhidi ya ufisadi, uhasama wa kikabila, umoja wa kitaifa, ugatuzi na suala la uchaguzi na jinsi linavyowaganya Wakenya kama njia ya kuhamasisha Wakenya kuhusu umoja wa kitaifa.

Ili kufanikiwa katika lengo hili, viongozi hawa walikubaliana kuunda afisi maalum itakayowajumuisha washauri ili kusaidia katika kufikia malengo yao.

Washirika wa Odinga kulalamika

Baada ya mkutano huo, washirika wa Bwana Raila Odinga katika muungano wa NASA, akiwemo Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula wamekuwa wakilalamika kuwa Raila Odinga, ambaye ni kiongozi wa muungano wa NASA, hakuwashirikisha wala kuwajulisha kuhusu mkutano wake na Rais Uhuru Kenyatta kabla ya mkutano huo kufanyika.

"Nasa ni muungano wa vyama vinne vikiwemo, Orange Democratic Movement (ODM), Wiper Democratic Movement-Kenya (WDM-K), Amani National Congress (ANC) na Ford Kenya," walisema katika taarifa.

Baadaye walipokutana washirika hawa wa upinzani, ilibainika kulikuwepo na kutoelewana kati ya Raila Odinga na wenzake. Walikubalina kwa pamoja kushauriana na vyama mbali mbali katika muungano huo kabla ya kuamua hatima ya muungano wao.

Baadaye, viongozi hao wengine wamekuwa wakisisitiza kuwa watafanya mkutano na Rais Uhuru Kenyatta ili kujadilaiana naye kuhusu masuala ya kitaifa, lakini baadaye serikali ilichukua hatua za kulegeza mkutano wake mkali dhidi ya viongozi hao.

'Nafuu kutoka kwa serikali ya Bw Kenyatta'

Tayari, baada ya mazungumzo haya kati ya Rais Kenyatta na Raila Odinga viongozi wa upinzani wamerudishiwa walinzi ambao walikuwa wameondolewa na serikali na baadhi yao kurudishiwa paspoti zilizokuwa zimetwaliwa na serikali.

Pia, viongozi wa upinzani wametangaza kusitishwa kwa mabunge ya maeneo ya kaunti maarufu kama People's Assembly ambayo yalikuwa yameundwa na muungano wa upinzani NASA kama mbinu mojawapo ya kutia shinikizo kwa serikali kukubali mazungumzo na upinzani.

Mkutano huu wa Rais Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga umepelekea matukio mengine ambayo wengi wanahofu utachangia kuvunjika kwa muungano wa vyama vya upizani, NASA.

Tayari viongozi wa vyama vingine tanzu katika muungano huu vimelalamikia uhusiano wa Rais Kenyatta na Bwana Raila Odinga jambo ambalo limepelekea kutoaminiana baina na kati ya washirika hawa wa muungano wa NASA.

Kuwabeza washirika

Siku chache zilizopita, washirika wa Bwana Raila Odinga wamekuwa wakionekana kutoa taarifa zinaoonyesha kuwabeza washirika wao katika upinzani.

Wachambuzi wa siasa za Kenya wanahoji kuwa hali ya sasa katika muungano wa upinzani, NASA, ni ishara tosha ya kuvunjika kwa muungano huo.

Wengine wanahoji kuwa wanasiasa mbali mbali katika muungano huo wameanza harakati za kujitayarisha kwa uchaguzi wa mwaka wa 2022.

Kando na kuchukua mwelekeo mpya kabisa katika siasa za Kenya, mkutano huu na matukio yanayouhusu yanakuja mwezi mmoja baada ya Bwana Raila Odinga aliyeshindwa katika uchaguzi wa Urais alipojiapisha kama "Rais wa wananchi".

Tukio hili la kujiapisha katika uwanja wa Uhuru Park ambapo washirika wengine wa upinzani hawakushiriki, lilizua maswali mengi katika siasa za Kenya maana lilikuwa kinyume cha sheria, kulingana na serikali ya Kenya.

Pia, lilianza kuonyesha ufa katika muungano wa NASA kwani baadhi ya wapinzani na washirika wao, walianza kuwaita viongozi wengine wa vyama tanzu katika NASA, "waoga".

Viongozi hao pamoja na Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula walichukua muda mwingi mwezi wa Februari mwaka huu kueleza ni kwa nini hawakushiriki katika hafla ya kumuapisha Raila Odinga.

Haki miliki ya picha AFP/Getty Images

Serikali ilijibu tukio hili kwa kufunga vituo vikuu vya runinga, kuwashika washirika wa upinzani na kumfurusha Wakili Miguna Miguna hadi Canada.

Hali iliyozuka baada ya tukio hili ilikuwa ya vitisho, wasiwasi na kupanda kwa joto la kisiasa nchini Kenya.

Hali hii ambayo ilitokea baada ya muda mrefu wa kisiasa za uchaguzi nchini imepelekea kuonekana kutokea kuelewana kati ya viongozi wa upinzani.

'Changamoto baada ya uchaguzi'

Sababu zinazopelekea hali hii ni kukosekana kwa raslimali na pesa za kuendeleza siasa za kupinga serikali katika muungano wa NASA, wanasiasa wa upinzani kutatizwa na kesi dhidi ya kuchaguliwa katika maeneo yao na ufadhili wa kifedha, na ukweli kwamba, baada ya siasa za muda mrefu katika historia ya Kenya, wanasiasa wengi wamekuwa fukara na wangependa kupata mdhamini.

Matukio makuu mzozo wa kisiasa Kenya

  • 8 Agosti, uchaguzi mkuu wafanyika ambapo Bw Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi
  • 1 Septemba, Mahakama ya Juu yabatilisha ushindi wa Bw Kenyatta katika kesi iliyowasilishwa na Bw Raila Odinga, na kuagiza uchaguzi urudiwe
  • 26 Oktoba, uchaguzi wa marudio wafanyika, huku upinzani ukisusia. Bw Kenyatta atangazwa mshindi.
  • 30 Januari, Bw Odinga ala kiapo kuwa 'Rais wa Wananchi' na kusisitiza kwamba hatambui Bw Kenyatta kama rais halali wa Kenya
  • 9 Machi, Bw Kenyatta akutana na Bw Odinga katika afisi ya rais Jumba la Harambee, wawili hao waahidi kushirikiana kuwaunganisha Wakenya.

Siasa za Kenya zina upekee wake pia. Siasa ndani ya muungano wa upinzani NASA, pamoja na haja ya wanasiasa humo kujiweka katika nafasi nzuri ya kuwania Urais mwaka wa 2022, ni mambo yanaoonekana kuelekea kuwatenganisha viongozi wa upinzani.

Chama tawala cha Jubilee pia kimekuwa kikitumia mbinu zote za kisiasa kuhakikisha kuwa umoja katika upinzani ni jambo adimu.

Zaidi ya haya, muungano wa upinzani Nasa, umepoteza uungwaji mkono katika nyanja za kimataifa kwani balozi za nchi nyingine nchini Kenya zimekuwa zikionekana kuwafokea kila mara katika juhudi zao.

Image caption Bw Wetangula amewahi kuhudumu kama waziri wa mambo ya nje

Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) ambacho ndicho chenye wabunge wengi wapinzani katika bunge la kitaifa, seneti na mabunge ya kaunti nchini Kenya kinaonekana kuchukua hatua ambazo zitasambaratisha muungano wa NASA.

Juma lililopita, chama cha ODM kiliwasilisha maombi katika bunge la seneti la Kenya kumwondoa kiongozi wa walio wachache katika bunge hilo Bw Moses Wetangula na kuwasilisha jina la seneta James Orengo kama kiongozi wa walio wachache katika bunge hilo.

'Dalili za kusambaratika'

Ingawa hatua hii haijaidhinishwa na spika wa bunge la Seneti, Ken Lusaka, ni dhahiri shahiri kuwa muda wa muungano wa upinzani unaelekea ukingoni.

Katika bunge la seneti la Kenya, kati ya maseneta wa upinzani 27, 20 ni wanachama wa ODM.

Wiper na ANC wana maseneta watatu kila mmoja, huku chama cha Ford Kenya kikiwa na seneta mmoja tu.

Tayari Seneta Moses Wetangula ambaye ni kinara-mwenza katika muungano wa Nasa amesema kuwa hali iliyopo katika muungano huo ni ya kusikitisha na itapelekea kusambaratika kwa muungano wao.

Amedokeza kwamba hatakubali kupokonywa nafasi hiyo kwa urahisi na kuwa kutengana kwa vyama vya Nasa kutakuwa safari ya mteremko.

Je, upinzani nchini Kenya utasambaratika kabisa ama muungano mpya utachipuka tena kulenga uchaguzi wa mwaka wa 2022? Je, hatima ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga katika ushirikiano wake na serikali itakuwa ipi?

Tukisubiri majibu ya haya siku zinavyosonga, kwa sasa ni wazi kwamba siasa za Kenya zinachukua mwelekeo mpya na mkondo wake.

Dkt Hezron Mogambi ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Nairobi

Mada zinazohusiana