Watoto wa mtaa duni Nigeria waliomvutia mwanamuziki Rihanna

The Ikorodu Talented Kids and Seyi Haki miliki ya picha The Ikorodu Talented Kids

Kundi la watoto wanaojiita Ikorodu ni watoto kutoka Nigeria ambao wanatumai kuwa maarufu duniani kupitia mchezo wa densi.

Wanaishi katika makazi duni ya eneo la Ikorodu jijini Lagos.

Kundi hilo lilianziwshwa mwaka 2014 ili kuwatoa watoto 'ombaomba' mitaani.

Hivi karibuni, video iliyowaonesha wakicheza ilivuma kwenye mitandao ya kijamii na kuwavutia nyota wakubwa wakiwemo Rihanna, mwanamitindo Naomi Campbell na Diddy.

Seyi Oluyole ni dada wa miaka 26 anayefanya kazi na watoto hao, kuwatoa mitaani na kuwaleta kwenye chumba cha mazoezi.

Yeye ndiye mwanzilishi wa 'The Dream Catchers', shirika linalowapatia watoto hao makazi wakiwa wanawafundisha jinsi ya kucheza.

"Nilipokwa kijana, nililala barabarani mara kadha kwa sababu ya matatizo ya kifedha ya familia," Seyi ameambia kipindi cha BBC NewsBeat

"Hapo ndipo nilipopenda kuwasaidia watoto wengine."

Ukurasa wao wa Instagram umejaa video nyingi za watoto hao wakicheza Nigeria kwa nyimbo za wanamuziki wa Afrobeat kama Wizkid na mwanamuziki wa Uingereza kama Big Shaq.

Watoto hao tisa wana umri kutoka miaka 6 hadi kumi na tano na hadi hivi karibuni hawakuwahi kulisikia jina la Rihanna.

Nyota wa kimataifa, Rihanna alisambaza video ya watoto hao kwa mashabiki wake milioni 60 wanaomfuata kupita ukurasa wake wa Instagram.

Alikuwa akisherekea kutajwa kama msanii aliyesikilizwa zaidi katika mtandao wa 'Apple music.'

Ndani ya muda mfupi nyota wengine walifuata hatua hiyo yake, Naomi Campbell akiandika, "MALKIA wacheza ngoma ... nasubiri sana kukutana nanyi ana kwa ana," katika ujumbe wake.

"Ukizingatia wametoka wapi, wengi wa watoto hawa hawakuwa wanawafahamu (wanamuziki hao nyota,2 anasema Seyi.

"Wazo hili kwamba mtu aliyeitazama video ni mtu maarufu sana katika taifa jingine ndilo lililowapendeza zaidi. Baadhi tulitokwa na machozi nilipowafafanulia maana yake.

"Wengi wetu tulitokwa na machozi kwa sababu ni kana kwamba wakati ambao tumekuwa tukiusubiri ulikuwa umewadia.

"Watu wametwambia kwamba tulikuwa tunapoteza muda wetu. Baadhi wamewaambia watoto hawa kwamba hawangefanikiwa."

Haki miliki ya picha The Ikorodu Talented Kids
Image caption Seyi (kati) anasema matamanio yake ni kwamba kila mtoto apate fursa sawa ya kufanikiwa

Lakini si umaarufu pekee waliokuwa wakiutafuta.

Seyi hutumia uchezaji ngoma kuwahamasisha watoto hao kuhakikisha kwamba wanafanya vyema shuleni.

"Watoto hawa hufanya mazoezi nyumbani na kwenye bustani iliyo karibu na nyumba," anasema.

"Siku ambazo huwa wanaenda shule, huwa twatumia saa moja hivi tukifanya mazoezi kwa kutegemea ufundi ambao unahitajika katika uchezaji ngoma ambao tunapanga kuutumia.

"Tunapenda kucheza ngoma sana, lakini iwapo hawafanyi vyema shuleni na kumaliza kazi wanayopewa na walimu basi hatutafanya mazoezi," anasisitiza.

Ikorodu Kids sisi watoto pekee wachezaji ngoma waliopata kutambuliwa kimataifa.

Mwaka jana, rapa French Montana alikwenda Kampala, Uganda na kuchezea video ya muziki wake kwa jina 'Unforgettable' na watoto wa chezaji ngoma wa Triplets the Ghetto Kids, ambalo ni kundi la watoto mayatima.

Video hiyo sasa imetazamwa mara 664 milioni kwenye YouTube, hatua inayoaminika kuchangia umaarufu wa wimbo huo.

Seyi anatumai kwamba Ikorodu Kids watafanikiwa vilevile.

"Watoto hao watakuwa watu maarufu sana.

"Kubadilisha ulimwengu kupitia ngoma na kuwa katika majukwaa maarufu kama vile Grammys, BET na MTV. Wanatumai pia watakutana na watu maarufu kama Serena Williams na Oprah," anasema.

"Ndoto yetu ni kwamba kila mtoto apate elimu bora, afikie ngazi ya Shahada au hata Shahada ya Pili. Tunatumai watoto hawa wanaweza kufikia ufanisi huu kupitia kujitolea kwao; uchezaji ngoma na uigizaji."