Cambridge Analytica yadaiwa kutumia maelezo ya watu Facebook kuwafaa wanasiasa

Alexander Nix Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Alexander Nix ambaye ni afisa mkuu mtendaji wa Cambridge Analytica

Vyama vya upinzani nchini Kenya vimeitisha uchunguzi kuhusiana na kampeini za uchaguzi mkuu wa mwaka uliopita, baada ya kampuni moja yenye makao yake jijini London, Cambridge Analytica, kudai kuwa ilihusika pakubwa na kampeni za uchaguzi ya zilizomfanya rais Uhuru Kenya kushinda mara mbili.

Kampuni hiyo ambayo imekana kutenda kosa lolote, pia inatuhumiwa kudukua data za kibinafsi za watumiaji milioni hamsini wa mtandao wa kijamii wa Facebook, ili kuingilia uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2016 nchini Marekani.

Vyama vya upinzani sasa vinataka uchunguzi kuhusiana na kile walichokitaja kama habari za kupotosha ili kuhujumu nia ya Wakenya kabla ya uchaguzi mkuu.

Kamishna wa mawasiliano wa Uingereza anatarajiwa kuomba kupatiwa hati ya upekuzi mahakamani ili kufanya upekuzi kwenye ofisi za kampuni hiyo ya Cambridge Analytica ambayo ina makao yake jijini London.

Wakuu wa Kampuni hiyo walinaswa na chombo cha Channel 4 wakisema kuwa watatumia mbinu za kuvutia, na rushwa ili kuwaaibisha wanasiasa.

Cambridge Analytica imekana shutuma hizo.


Kujiondoa Facebook ndiyo dawa?

Baada ya kuibuka kwa tuhuma hizo, baadhi ya watu mtandaoni wameanza kuwahimiza wenzao wajiondoe Facebook au kufuta akaunti zao za Facebook.

Wametumia vitambulisha mada #DeleteFacebook (Ifute Facebook) au #BoycottFacebook (Gomea/Susia Facebook).

"Sote tulihama na kuisahau MySpace. Mnaweza kuihama Facebook pia."


Hayo yakijiri, afisa mkuu mtendaji wa Facebook Mark Zuckerberg ametakiwa kufika mbele ya kamati moja ya bunge Uingereza kutoa ushahidi kuhusu uhusiano wa kampuni hiyo na Cambridge Analytica.

Mbunge Damian Collins, anayeongoza uchunguzi kuhusu ueneaji wa habari za uzushi, ameituhumu Facebook kwa kutoa "taarifa za kupotosha kwa kamati" hiyo wakati wa kikao cha awali ambacho kilikuwa kinachunguza ni habari za aina gani ambazo zilichukuliwa kutoka kwa mtandao huo bila idhini ya watumiaji wa mtandao huo.

Shutuma

Siku ya Jumatatu, Channel 4 ilirusha picha za kamera za siri zilizomuonyesha Mkurugenzi Alexander Nix akieleza mbinu za Kampuni yake ambazo angezitumia kuwafedhehesha wanasiasa mitandaoni.

Kwenye picha za kamera alionekana akipendekeza njia moja wapo ni ''kuwaahidi donge nono na kuhakikisha kuwa wanarekodiwa picha za video''.

Haki miliki ya picha Channel 4 News
Image caption Alexander Nix (kulia) anadaiwa kuoneshwa kwenye ufichuzi wa Channel 4

Pia alisema anaweza ''kuwapeleka wasichana mpaka kwenye nyumba za wagombea'' akiwasifia ''wanawake wa Ukraine ni warembo sana, mpango huo utafanikiwa vizuri sana''.

Bwana Nix aliendelea ''Ninawapa tu mifano ya yale yanayoweza kufanywa na yaliyofanywa''.

Hata hivyo,Kampuni hiyo imesema ripoti iliyotolewa dhidi yao na mazunguzo yaliyonaswa kwenye kamera ni ya ''uongo mtupu''

''Cambridge Analytica haijihusishi na vitendo vya rushwa wala mitego ya kushawishi'' ilisema.

Nix alikiambia kipindi cha Newsnight cha BBC kuwa anaiona ripoti hiyo kuwa ni ya ''kupindisha ukweli'' na anaamini kuwa Kampuni yake ''inafanyiwa hila za makusudi''

Kamishna wa habari wa Uingereza, Elizabeth Denham anachunguza Kampuni hiyo kutokana na madai yaliyotolewa dhidi yake ya kutumia data za watu binafsi kufanya ushawishi kwenye uchaguzi wa Marekani.

Bi Denham ametaka kuziona data na kuzikagua.

Amesema Ofisi yake imekuwa ikichunguza kampeni za kisiasa na matumizi ya data za kisiasa kwa miezi mingi, madai dhidi ya Facebook na Cambridge Analytica ni moja wapo

Amesema anafanya uchunguzi kubaini kama data zilitumika baada ya kuidhinishwa, kama walipata ruhusa ya kutumia data hizo, na kitu gani kilichofanyika kuzihakikishia usalama wake na kama Facebook ilichukua hatua baada ya kubaini kupotea kwa data.

Bi Denham alikiri kuwa aliiambia Facebook ijiondoe kwenye upekuzi wake kwenye Ofisi za Cambridge Analytica, kwa sababu unaweza kuharibu uaminifu katika uchunguzi wake.

''Tuliishauri Facebook iachane na uchunguzi wao na wamekubali'', aliiambia Radio 4 ya BBC.

Waziri kivuli kutoka Chama cha Labour, Liam Byrne amesema Denham alishindwa kuomba waranti kimyakimya badala yake aliuambia ulimwengu kuwa nakwenda mahakamanni,''na kuipa nafasi Cambridge Analytica na wengine kuficha ushahidi, alikiambia kipindi.

Haki miliki ya picha AFP

Denham amesema atatumia mamlaka zote alizonazo kwa mujibu wa sheria lakini hafahamu kama ushahidi umefichwa mpaka pale timu yake itakapopata kibali cha kuingia kwenye Ofisi hizo.

Kukiuka taratibu

Cambridge Analytica inasisitiza kuwa ilifuata taratibu zote katika kupata Data, lakini iliondolewa kutoka Facebook wiki iliyopita.

Facebook, wakati huo huo, itafanya mkutano wa wazi na wafanyakazi wake baadae kujadili jambo hilo.

Facebook imesema imeajiri timu ya kuikagua Cambridge Analytica kubaini kama Data ya Facebook inayojadiliwa bado ipo.

Ikiwa Data hiyo itabainika kuwepo, utakuwa ni ukiukaji mkubwa wa sera za Facebook na kuvunja uaminifu kwenye makundi hayo.

Nako nchini Kenya, Upinzani nchini humo umetaka Kampeni za mwaka jana za uchaguzi zifanyiwe uchunguzi baada ya Cambridge Analytica kusema kuwa zimeshiriki kuwa sehemu muhimu ya ushindi mara mbili wa Rais Uhuru Kenyata.

Upinzani nchini Kenya unataka ufanyie uchunguzi kile wanachodai kuwa Kampeni za kubadilisha matakwa ya raia wa Kenya.

Delano Kiilu, ambaye ni katibu mkuu wa chama cha kuhifadhi data, Protective and Safety Association of Kenya (PROSAK). amesema itabidi uchunguzi wa hali ya juu ufanywe kabla ya kuitia hatiani kampuni ya Cambridge Analytica.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii