Josephine Majani: Mwanamke aliyedhalilishwa akijifungua Bungoma, Kenya kulipwa $25,000

Furaha ya Majani Haki miliki ya picha Fredrik Lerneryd

Mahakama Kuu nchini Kenya imeamuru mwanamke aliyeteswa na kudhalilishwa wakati wa kujifungua hospitalini alipwe fidia ya jumla ya dola 25,000 za Marekani.

Mwanamke huyo alidhalilishwa miaka mitano iliyopita katika kisa ambacho kilizua lalama kutoka kwa raia na watetezi wa haki za kibinadamu baada ya kuangaziwa kwenye vyombo vya habari na mtandaoni.

Jaji wa mahakama kuu ya Bungoma, magharibi mwa Kenya, Abida Aroni alisema mamlka ya afya nchini Kenya ilikiuka haki za kimsingi za Josephine Majani alipotengwa na kukosa kuhudumiwa wakati wa kujifungua katika hosipitali ya umma mwaka 2013.

Jaji huyo alisema kuwa haki za kimsingi za afya za Bi Majani, pamoja na heshima yake vilikiukwa kupitia yeye kuteswa kimwili na kutusiwa na wauguzi katika hospitali ya Bungoma.

Na kutokana na hilo, akaamuru alipwe fidia ya dola alfu 25.

Bi Majani amefurahia uamuzi huo akisema kuwa haki hatimaye imetendeka.

Aliyoyapitia Josephine mikononi mwa wauguzi hao yalipata kujulikana baada ya mtu kurekodi video kwenye simu yake na kuipakia kwenye mtandao wa kijamii.

Bw Martin Onyango, wakili wa Josphine kutoka kituo cha Afrika kuhusu afya ya uzazi anasema kuwa kesi hii ni ushindi mkubwa kwa wanawake wanaotafuta huduma bora za afya ya uzazi katika hospitali za umma nchini Kenya.

Mwandishi wetu Victor Kenani aliyepo Nairobi anasema visa vinavyohusiana na unyanyasaji vimekuwa vikiripotiwa mara kwa mara katika hospitali za umma nchini Kenya.

Haki miliki ya picha HISANI/Fredrik Lerneryd
Image caption Bi Majani (Kati) anapanga kutumia pesa atakazolipwa fidia kumlea mwanawe

Bi Majani amesema fidia hiyo itamsaidia kumlea mtoto ambaye karibu ampoteze wakati wa kujifungua.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu idadi ya watu, wanawake 495 kati ya laki moja walio wajawazito hufa kila mwaka kutokana na matatizo wakati wa kujifungua.

Shirika hilo linasema uamuzi wa leo umetoa mwongozo kuwa lazima wapewe huduma ya kujifungua ya viwango vya juu iwepo ili kuzuia vifo vya aina hiyo kutendeka.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii