Misri yazindua mtandao wake wa kijamii, EgFace

Mtandao huu mpya hauungwi mkono na walio wengi nchini Misri
Image caption Mtandao huu mpya hauungwi mkono na walio wengi nchini Misri

Mtandao mpya wa kijamii unaofanana na Facebook umezinduliwa nchini Misri, kwa jina la EgFace.

Mtandao wa An-Nahar wamesema mtandao huo unaelekea kuwa uliundwa kwa haraka sana, kwa kipindi cha chini ya majuma mawili baada ya Waziri wa mawasiliano nchini Misri kutangaza kuwa Misri itazindua mtandao wake wa kijamii.

Raia wa Misri walionyesha kukejeli na kutounga mkono uamuzi huo uliotangazwa tarehe 12 mwezi Machi, wengi wao wakiwa na mawazo kuwa, hatua hiyo ni ya makusudi kuwezesha vyombo vya usalama kufuatilia watumiaji wa mtandao huo , kukusanya taarifa na kufuatilia anuani za watumiaji.

Anuani nyingi za Facebook zimefungwa nchini Misri hivi karibuni na wengine wamekamatwa kwa makosa ya ''uchochezi'' dhidi ya serikali ya Misri,Jeshi na Polisi.