Tanzania: Mbowe na maafisa wengine wa Chadema wasomewa mashtaka

Freeman Mbowe Haki miliki ya picha CHADEMAMEDIA / TWITTER
Image caption Kiongozi wa Chadema Freeman Mbowe (kulia) ni mmoja waliosomewa masktaka

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na viongozi wengine wa chama hicho wameelezwa mashtaka 8 katika mahakama ya Kisutu kuhusiana na maandamano.

Viongozi hao wa upinzani wamesomewa mashtaka mbele ya Hakimu mkazi wa Kisutu Wilbard Mashauri.

Wakili wa serikali Faraja Nchimbi amedai kosa lao la kwanza ni kuandaa mikusanyiko ama maandamano yasiyo na uhali.

Miongoni mwa mashtaka waliyosomewa ni pamoja na maandamano yaliyosababisha kifo cha mwanafunzi wa chuo cha NIT Akwilina Akwiline.

Wanashtakiwa pia kuendelea kufanya mkusanyiko usio halali wilayani Kinondoni linalowakabili washtakiwa wote.

Wakili Nchimbi amedai kuwa kosa jingine ni ambalo linamlenga Bwana Mbowe ni kuhamasisha chuki miongoni mwa jamii.

Mbowe anashtumiwa pia kwa makosa ya kuchochea na kushawishi chuki miongoni mwa waTanzania dhidi ya uongozi uliopo madarakani.

Washtakiwa wote walikana mashtaka yote dhidi yao ambapo Wakili Nchimbi amedai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na anaomba tarehe kwa ajili ya kuwasomea maelezo ya awali.

Viongozi wengine wa upinzani waliosomewa mashtaka ni pamoja na Bwana Msigwa.

Wakili Nchimbi ameiomba mahakama hiyo iwanyime washtakiwa dhamana kwa sababu za usalama.

Chadema kimelaani vikali kukamatwa kwa viongozi wao: ''Zimekua ni sarakasi dhidi ya upinzani...njama hizi dhidi viongozi wetu hatutaweza kuzinyamazia, tutaendelea kuzilaani na tunaangalia uwezekano wa kuchukua hatua za kisheria'' Afisa habari wa Chadema Tumaini Makene ameileza BBC.

Bwana Makene amesema viongozi wa Chadema ambao wamekuwa wakiripoti polisi kwa tarehe zilizokuwa zimepangwa, ilikuwa ni siku yao ya kufika kituo cha Polisi.

Hata hivyo amesema kuwa Chadema haifahamu sababu za kukamatwa kwao na kunyimwa dhamana.

Mada zinazohusiana