Marufuku za utawala wa Rais Magufuli Tanzania

Rais wa Tanzania John Magufuli Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais wa Tanzania John Magufuli

Rais wa Tanzania,John Magufuli ameonekana kuwa ni kiongozi anayetoa maamuzi ya haraka kwa kutoa marufuku ya jambo au kuwaachisha kazi watendaji katika nyadhifa zao.

"Kutumbua majipu" ni neno ambalo limekuwa maarufu katika vinywa vya wengi baada ya kiongozi huyo kuwafukuza kazi watendaji pale ambapo anaona mambo hayaendi sawa.

Mfano hivi karibuni, Rais Magufuli amewaachisha kazi wakurugenzi wawili mkoani Kigoma mara tu baada ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kumkabidhi ripoti ambayo ilikuwa na matokeo mabaya katika eneo hilo.

Lakini haya chini ni orodha ya marufuku aliyoyatoa Rais Magufuli yanaoathiri sekta mbali za serikali ya Tanzania tangu aingia madarakani;

Maandamano na mikutano ya Kisiasa

Image caption Polisi wamekuwa wakitahadharisha juu ya maandamano mara kwa mara

Rais Magufuli amenukuliwa akisema shughuli za siasa ikiwa ni pamoja na maandamano na mikutano ya hadhara isimame hadi uchaguzi ujao mwaka 2020.

Amedai baada ya uchaguzi uliopita, "sasa ni wakati wa kazi tu"

Vyombo vya usalama vimekuwa vikitahadharisha mara kwa mara kuwa hawatasita kumchukulia hatua kali za kisheria mtu yeyote au chama chochote cha siasa kitakachokaidi agizo hilo.

Aidha maafisa hao wamewataka wananchi kuwa makini na wanasiasa wenye lengo la kutaka kuvuruga amani ya nchi na badala yake kuwasihi waendelee kushirikiana katika kujenga Umoja wa taifa la Tanzania.

Hata hivyo, maafisa hao kupitia vyanzo vyao mbalimbali vya habari wamebaini kuwa mikutano hiyo ina lengo la kuwahamasisha wananchi kutotii sheria za nchi.

Shughuli za siasa, ikiwa ni pamoja na kufanya mikutano ya hadhara na maandamano ni haki ya raia kwa mujibu wa katiba ya Tanzania.

Usafirishwaji wa madini nje ya nchi

Haki miliki ya picha IKULU
Image caption Rais Magufuli akihesabu makontena yenye mchanga wenye madini alipofanya ziara ya kushtukiza Machi 2017

Mwaka jana, Rais Magufuli alipiga marufuku usafirishwaji wa madini yasiyo chenjuliwa mpaka pale kodi za nyuma ziwe zimelipwa.

Serikali hiyo iliweka mpango wa utaratibu utakaowezesha ujenzi wa kiwanda cha uchenjuaji wa makinikia yaani Smelter, hapa nchini ili kudhibiti upotevu wa mapato na kutengeneza mapato kwa watanzania.

Waliopata mimba shuleni wasirejee shule

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wanafunzi watakaopata ujauzito wakiwa shuleni hawataruhusiwa tena kurudi shuleni

Rais Magufuli alisema kuwa chini ya uongozi wake wanafunzi wa kike ambao watakaopata ujauzito wakiwa shuleni hawataruhusiwa tena kurudi shuleni.

Aidha Magufuli alikumbusha kwamba sheria inasema mwanaume ambaye atapatikana na hatia ya kumpa mimba mtoto wa shule, atafungwa jela miaka 30.

Magufuli aliongeza kwamba mwanaume huyo atapata fursa ya kutumia nguvu alizotumia kumpachika mimba msichana huyo, kufanya kilimo akiwa gerezani.

Nchini Tanzania kuna takriban wasichana 8,000 ambao huacha shule kila mwaka kutokana na kuwa wajawazito, kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Human Rights Watch.

Usajili wa meli mpya

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Miongoni mwa meli za kigeni zilizosajiliwa Tanzania

Miongoni mwa mambo ambayo yamepigwa marufuku nchini Tanzania tangu rais Magufuli aingie madarakani ni pamoja na kusitisha usajili wa meli mpya nchini humo 'mpaka itakapotangazwa vinginevyo'.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, Rais Magufuli aliagiza utoaji wa vibali na usajili usimame hadi hapo uchunguzi kina ufanyike kwa meli zote 470 ambazo zimesajiliwa Tanzania na zinapeperusha bendera ya Tanzania.

Agizo hilo lilikuja baada ya taarifa za kukamatwa kwa meli zilizokuwa zimepakia shehena za dawa za kulevya na silaha huku zikiwa zinapeperusha bendera ya Tanzania.

Mbali na marufuku hizo ambazo zimetolewa na yeye mwenyewe zipo nyingine ambazo zimetajwa wakati wa utawala wake.

Shisha

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption shisha

Serikali ya Tanzania imepiga marufuku uvutaji wa shisha nchini humo na kulitaka jeshi la polisi kufanya kila juhudi kutokomeza uraibu huo.

Image caption Uvutaji wa shisha ni marufuku Tanzania

Katazo la mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam bwana Paulo makonda lilifuatiwa na lile la Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ambapo alitoa agizo na kusema uvutaji shisha umekuwa ukichangia katika kudorora kwa maadili miongoni mwa vijana, na kuwapunguzia uwezo wa kiakili na kimwili wa kufanya kazi.

Viroba

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kenya wakiteketeza pombe haramu 2015

Mapema mwaka jana,pombe zilizokuwa zinauzwa kwenye mifuko midogo ya plastiki zimepigwa marufuku kuuzwa katika maeneo yeyote nchini humo.

Serikali yapiga marufuku viroba Tanzania

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii