Waziri mkuu Kassim Majaliwa awasihi viongozi wa kidini wakumbatie amani

Waziri Mkuu wa Tanzania Bwn Kassim Majaliwa
Maelezo ya picha,

Waziri Mkuu wa Tanzania Bwn Kassim Majaliwa amesema serikali inatambua umuhimu wa dini

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewaomba viongozi wa dini popote walipo wahakikishe wanaipigania na kuilinda amani kwa kila hali ikiwani pamoja na kupambana na viashiria vya uvunjifu wa amani.

Wito huu unatolewa siku chache baada ya baadhi ya makanisa ya kikristo kukosoa utendaji wake.

Kanisa la Kilutheri nchini Tanzania

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Katika waraka wa ujumbe wa pasaka uliosambaa katika mitandao ya kijamii , baraza hilo liliorodhesha mambo kadhaa ambayo wameyataja kuwa ndio tishio la umoja na amani

Baraza la maaskofu wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri chini Tanzania (KKKT) kusema kuwa Umoja na amani ya Tanzania viko hatarini.

Katika waraka wa ujumbe wa pasaka uliosambaa katika mitandao ya kijamii , baraza hilo liliorodhesha mambo kadhaa ambayo wameyataja kuwa ndio tishio la umoja na amani ya nchi hiyo.

Waraka uliyataja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na utekaji, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi.

Ujumbe huo kutoka baraza la maaskofu wa KKKT ulitolewa siku chache tu baada ya ujumbe wa Kwaresima uliotolewa na baraza la Maaskofu wa kanisa Katoliki.

"Shughuli za kisiasa kama vile maandamano, mikutano ya hadhara, ambayo ni haki ya kila raia, vinaendelea kuzuiwa kwa kutumia vyombo vya dola", ilieleza sehemu ya waraka huo wa Maaskofu wa kanisa Katoliki

Akizungumza na viongozi wa kiislam Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) jijini Dodoma, Waziri Mkuu Majaliwa amesema serikali inatambua umuhimu wa dini: ''dini ni taasisi muhimu sana kwa maisha yetu ya kila siku ndio maana Serikali inaheshimu na kuzitambua dini zote kutokana na mchango wake mkubwa katika amani ya nchiyetu. Niwaombe viongozi wangu popote mlipo muilinde amani yetu''

Waziri Mkuu huyo ameongeza kusema kuwa, ahadi ya Rais Dkt.Magufuli ni kuwa Serikali anayo iongoza ipo tayari kusikiliza maoni,ushauri na mapendekezo yeyote kutoka kwaviongozi wa dini.'milango iko wazi saa zote'.

Serikali ya rais John Pombe Magufuli imekuwa ikisifiwa kwa kudhibiti ufisadi, lakini wakosoaji wake wanailamu kwa utekaji, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya upinzani , mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi.