Tiangong-1: Chombo cha anga za juu cha China chaanguka Pacific

Radar image of Tiangong

Chanzo cha picha, FRAUNHOFER

Maelezo ya picha,

Chombo hicho cha China kwa jina Tiangong-1 kilifuatiliwa kwa mitambo ya rada

Chombo cha anga za juu cha China kilichoacha kutumika Tiangong-1 kimemeguka vipande vingi kikiingia anga ya dunia na kuanguka maeneo ya bahari kusini mwa Pacific.

Chombo hicho kiliingia anga ya dunia saa 00:15 GMT Jumatatu, idara ya anga za juu ya China imetangaza.

Tiangong-1 ilirushwa angani mwaka 2011 kufanyia majaribio teknolojia ya kuunganisha vyombo mbalimbali anga za juu na pia vyombo vya kuzunguka kwenye mzingo wa dunia.

Chombo hicho ni sehemu ya juhudi za China za kuunda kituo cha anga za juu kitakachokuwa kinadhibitiwa na binadamu katika anga za juu kufikia mwaka 2022.

Kiliacha kufanya kazi Machi 2016.

Tunayoyafahamu kuhusu eneo ambalo kilianguka?

Maafisa wanasema tu kwamba kilianguka "juu ya Pacific Kusini".

Wataalamu wa anga za juu wa Marekani wamesema wametumia teknolojia ya kufuatilia mzingo wa dunia kuthibitisha kuingia ardhini kwa Tiangong-1.

Mtaalamu wa anga za juu Jonathan McDowell kutoka Harvard ameandika kwenye Twitter kwamba huenda chombo hicho kimeanguka kaskazini magharibi mwa Tahiti.

Wataalamu walitatizika kubaini hasa ni wapi chombo hicho kingeanguka.

Idara ya anga za juu ya China ilikuwa awali imekadiria kimakosa kwamba chombo hicho kingeanguka karibu na Sao Paulo, Brazil muda mfupi kabla ya chombo hicho kuingia anga ya dunia.

Shirika la Anga za Juu la Ulaya lilisema mapema kwamba uwezekano mkubwa ni kwamba chombo hicho cha Tiangong-1 kingeanguka baharini.

ESA walisisitiza kwamba uwezekano wa mtu kugongwa na vifusi vhya vyombo hicho ulikuwa "chini ya mara milioni kumi ya uwezekano wa mtu kupigwa na radi."

Haijabainika ni kiasi gani cha vifusi hivyo kimeanguka ardhini.

Mbona chombo hiki kikaanguka hivi?

Tiangong kilifaa kusitisha shughuli yake ya kuizunguka dunia kwa utaratibu na mpangilio fulani.

Ni chombo kilichokuwa na urefu wa mita 10 (futi 32) na uzani wa zaidi ya tani 8 na ni kikubwa zaidi ya vyombo vyote vilivyoundwa na binadamu ambavyo vimewahi kuanguka kutoka anga za juu.

Lengo lilikuwa kutumia vifaa vinavyokipa chombo hicho msukumo kukielekeza hadi maeneo ya mbali yasiyo na watu maeneo ya Bahari ya Kusini.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

China ilikituma chombo cha Tiangong-1 angani mnamo 2011

Lakini kabla ya hilo kufanyika, ghafla mfumo wa kukidhibiti ulikumbwa na hitilafu na wataalamu wa China wakapoteza udhibiti.

Mashirika 13 ya anga za juu ya mataifa mbalimbali, yakiongozwa na Shirika la Anga za Juu la Ulaya (ESA), yalifuatilia njia ya Tiangong na kujaribu kuiga tabia yake kadiri kilivyokaribia kuingia ndani ya anga ya dunia huku kikiendelea kuizunguka.

Tiangong maana yake ni 'Kasri la Mbinguni'

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mwanananga Wang Yaping alitoa mhadhara unaokumbukwa sana kwa watoto akiwa moja kwa moja kutoka chombo cha Tiangong-1 kikiwa anga za juu

  • Chombo hiki kirirushwa mwaka 2011 kufanyia majaribio utaratibu wa kutuma vyombo vingine na kuviunganisha vikiwa anga za juu
  • Makundi mawili ya wanaanga yalizuru chombo hicho wakitumia vyombo vidogo kwa jina Shenzhou - mwaka 2012 na 2013
  • Walijumuisha wanaanga wa kwanza wa kike kutoka China Liu Yang na Wang Yaping
  • China inapanga kutuma chombo cha anga za juu cha kudumu katika mwongo mmoja ujao
  • Imeunga roketi inayobeba kuinua vitu vya uzani wa juu sana kwa jina Long March 5 kwa ajili ya kazi hiyo

Ndicho chombo kikubwa zaidi kuwahi kuanguka kutoka angani?

Tiangong ni miongoni mwa vyombo vingine vikubwa vilivyowahi kuanguka bila kudhibitiwa, lakini bado kineachwa nyuma na vyombo vingine.

Chombo cha Skylab cha Marekani kilikuwa na uzani wa tani 80 kilipoanguka, ingawa kiliweza kudhibitiwa kwa kiasi fulani, mwaka 1979.

Kilianguka Australia Magharibi ardhini lakini hakuna aliyejeruhiwa.

Chombo cha Nasa cha Columbia nacho kilikuwa na uzani wa tani 100 kilipoanguka mwaka 2003.

Tena, ardhini hakuna aliyegongwa na vifusi vyake ambavyo vilitapakaa majimbo ya Texas na Louisiana.

Mtaalamu Jonathan McDowell kutoka Kituo cha Fizikia ya Anga za Juu cha Harvard-Smithsonian anasema kwa kukadiria, 50 ni chombo cha 50 kwa ukubwa.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Mchina wa kwanza aliyefanya safari ya anga za mbali 2003 alikuwa shujaa wa taifa

Je Tiangong-ni nini?

Uchina ilichelewa kuanza uvumbuzi wake wa anga za juu.

Mnamo 2001, Uchina ilizindua vyombo vyake vya anga kwa kujaribu kuwatuma wanyama mwaka 2003 kwenye chombo cha anga za mbali kwenye mzingo wa dunia, na hivyo kuifanya nchi hiyo kuwa ni ya tatu kufanya hivyobaada ya Muungano wa Usovieti na Marekani.

Mpango wa vituo vya safari za anga za mbali ulianza kwa kukituma chombo cha Tiangong-1 ama "Kasri la Mbinguni", mwaka 2011.

Kituo hicho kidogo kiliweza kuwahifadhi wataalam wa masuala ya anga za mbali lakini kwa muda mfupi wa siku kadhaa. Mchina wa kwanza mwanamke mtaalamu wa anga za juu Liu Yang alitembelea kituo hicho mwaka 2012.

Kilikamilisha huduma zake mwezi Machi 2016, miaka miwili zaidi ya muda kiliopangiwa.