Matiang'i: Miguna lazima aombe tena uraia wa Kenya ili aruhusiwe kuingia kama raia

Matiang'i

Waziri wa mambo ya ndani nchini Kenya Dkt Fred Matiang'i amesema mwanasiasa wa upinzani aliyetimuliwa nchini humo Miguna Miguna atalazimika kuomba tena uraia.

Waziri huyo amesema Bw Miguna alipoteza uraia wake alipouchukua uraia wa Canada mwaka 1988 na hawezi kuruhusiwa kuingia nchini Kenya kama raia bila kuomba tena uraia.

Dkt Matiang'i, aliyekuwa akihojiwa na kamati ya bunge, amesema mwanasiasa huyo ambaye pia ni wakili alijipatia paspoti yake ya Kenya na kitambulisho cha taifa anachokitumia kwa sasa kwa njia ya ulaghai.

Waziri huyo amesema hakuna shaka kwamba Bw Miguna alizaliwa Kenya.

"Yeyote aliyechukua uraia wa taifa jingine kabla ya katiba ya sasa kuidhinishwa mwaka 2010 ambaye anafikiri kwamba ataweza kurejea bila kufuata utaratibu uliowekwa anajihadaa.

"Hapana shaka kwamba Miguna alizaliwa Kenya. Lakini kwa mujibu wa katiba ya kabla ya 2010, yeyote aliyechukua uraia wa nchi nyingine alipoteza uraia wake wa Kenya. Bunge liliidhinisha sheria inayoeleza jinsi mtu kama huyo anavyoweza kuupata tena uraia wake."

Waziri huyo pia amejitetea dhidi ya shutuma kwamba amekuwa akikaidi maagizo ya mahakama ya kutaka Bw Miguna aachiliwe huru na kuruhusiwa kuingia Kenya.

Jaji wa Mahakama Kuu George Odunga alikuwa ameagiza Dkt Matiang'i, pamoja na mkuu wa polisi Joseph Boinnet, mkuu wa idara ya uhamiaji Gordon Kihalangwa na katibu wa wizara ya mambo ya ndani Karanja Kibicho wafike mbele yake kueleza ni kwa nini walikosa kutekeleza amri ya mahakama ya kumruhusu Bw Miguna aingie Kenya.

Dkt Matiang'i amesema: "Jaji alipokuwa anatutaka tufike mbele yake tulikuwa tunahudhuria sherehe za kufuzu kwa maafisa wa polisi wa kukabiliana na fujo (GSU). Tulihukumiwa bila kupewa fursa ya kujieleza, kwa kutumia madai ya uongo."

Jaji Odunga aliwapiga faini maafisa hao Sh200,00 kila mmoja, na akaagiza pesa hizo zikatwe kutoka kwa mishahara yao.

Dkt Matiang'i pia amepuuzilia mbali madai kwamba serikali ilimfurusha Bw Miguna kutoka nchini humo akisema hatua kama hiyo ingehitaji idhini yake.

Chanzo cha picha, AFP/Getty

Maelezo ya picha,

Miguna aliwasili uwanja wa JKIA Jumatatu wiki iliyopita lakini akazuiwa kuingia nchini Kenya

"Hakufurushwa kutoka Kenya. Nilihitaji kutia saini idhini ya kumfurusha. Hatungemfurusha kwani hakuwa ameingia bado ndani ya eneo la utawala wetu," Dkt Matiang'i amesema.

"Tulimuondoa uwanja wa ndege kama mtu ambaye hakuwa na stakabadhi za kumtambua, abiria ambaye hangetambuliwa ambaye kawaida hurejeshwa alikotoka."

Waziri huyo amesema Miguna hataruhusiwa kurejea Kenya bila kuomba kurejeshewa uraia wa Kenya.

Katiba ya kabla ya 2010 haikuruhusu uraia wa nchi mbili kama ilivyo kwa katiba ya sasa.

Kukamatwa kwa Miguna mara ya kwanza

Bw Miguna alikamatwa na polisi kwa mchango wake katika kuapishwa kwa Bw Odinga kuwa "rais wa wananchi", hafla iliyofanyika uwanja wa Uhuru Park, Nairobi mnamo 30 Januari.

Bw Miguna, ambaye pia ni wakili, ndiye aliyetia saini hati ya kiapo ya Bw Odinga.

Serikali ilikuwa imeeleza hatua hiyo ya kiongozi huyo wa upinzani kuwa uhaini wa hali ya juu.

Bw Odinga anadai kwamba alimshinda Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu wa 8 Agosti ambao matokeo yake yalifutiliwa mbali na Mahakama ya Juu kwa sababu ya kutokea kwa kasoro nyingi.

Mahakama iliamuru uchaguzi mpya ufanyike lakini Bw Odinga akasusia uchaguzi huo mnamo 26 Oktoba.

Chanzo cha picha, HISANI

Maelezo ya picha,

Bw Miguna alisambaza picha anazosema ni zake akiwa hospitalini kumuona daktari uwanja wa ndege Dubai punde baada ya kufikishwa Dubai

Aliyezaliwa Kenya anaweza kupoteza uraia?

Chini ya Kifungu 17 cha Katiba ya Kenya, mtu aliyezaliwa nchini Kenya anaweza tu kuupoteza uraia wake iwapo itabainika kwamba aliupata uraia huo kwa njia ya ulaghai, au ibainike kwamba mtu huyo au wazazi wake walikuwa raia wa nchi nyingine, au ibainike kwamba mtu huyo alikuwa na umri wa zaidi ya miaka minane alipogunduliwa akiishi Kenya.

Serikali ya Kenya imekuwa ikisisitiza kwamba chini ya katiba ya zamani, Wakenya hawangekuwa na uraia wa nchi mbili.

Serikali inasema hatua ya Bw Miguna ya kupata pasipoti ya Canada mwaka 1988 ina maana kwamba aliupoteza uraia wa Kenya wakati huo.

Ingawa Bw Miguna aliwasilisha maombi na akapewa pasipoti ya Kenya mwaka 2009, serikali inasema pasipoti hiyo ya Kenya si halali kwa sababu hakufichua kwamba wakati huo alikuwa raia wa Canada pia.

Serikali imesema mwanasiasa huyo hakuwasilisha tena ombi la kuruhusiwa kuwa raia wa Kenya katiba ilipofanyiwa marekebisho mwaka 2010 na Wakenya wakakubaliwa kuwa na uraia wa nchi mbili.

Bw Miguna amekuwa akisisitiza kwamba hakuwahi kuukana uraia wake wa Kenya na kamwe hawezi kufanya hivyo.

"Katiba iko wazi kabisa: hakuna mtu yeytoe anayeweza au anayeweza kudai kuufuta uraia wa Mkenya aliyezaliwa nchini Kenya," alisema awali.

Matukio makuu mzozo kuhusu Miguna

30 Januari: Miguna aidhinisha hati ya kiapo cha Raila Odinga kuwa 'Rais wa Wananchi'

2 Februari: Atangaza kwamba amekamatwa na polisi Nairobi

6 Februari: Afurushwa kutoka Kenya na kupelekwa Canada

16 Machi: Odinga waambia wafuasi wake kwamba baada ya mapato yake na Bw Kenyatta, Miguna anafaa kuruhusiwa kurejea Kenya bila masharti

26 Machi: Arejea Kenya lakini azuiliwa uwanja wa ndege wa JKIA. Baadaye usiku, anusurika jaribio la kumpeleka Dubai.

28 Machi: Miguna apelekwa Dubai kwa nguvu.

02 Aprili: Miguna asafiri kutoka Dubai kwenda Canada

Miguna Miguna ni nani?

Miguna alizaliwa katika kijiji cha Magina, katika jimbo la Kisumu, magharibi mwa Kenya.

Bw Miguna amekuwa kiongozi wa kundi linaloitwa National Resistance Movement (NRM, Vuguvugu la Taifa la Kupinga Serikali), ambalo liliundwa na muungano wa upinzani wa National Super Alliance siku moja kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa marudio ambao Bw Odinga alisusia mnamo 26 Oktoba mwaka jana.

"Utakuwa ni muungano wa ukombozi," alisema Bw Odinga akitangaza kuundwa kwa vuguvugu hilo.

"Tumesema hatutaheshimu serikali dhalimu."

Bw Miguna baadaye alijitangaza kuwa Jenerali wa NRM.

Mnamo 30 Januari, siku ya kuapishwa kwa Bw Odinga kuwa 'Rais wa Wananchi', muungano huo uliorodheshwa kuwa kundi haramu na waziri wa usalama Dkt Fred Matiang'i.

Hiyo haikuwa mara ya kwanza kwa Bw Miguna kujipata akikabiliana na serikali na nguvu zake.

Mwaka 1988, alikamatwa na serikali ya wakati huo ya Rais Daniel arap Moi.

Bw Miguna baadaye alitorokea Kenya ambapo alipata hifadhi kama mkimbizi wa kisiasa.

Alirejea nchini Kenya na akashiriki katika kampeni za uchaguzi za Bw Odinga na chama chake cha Orange Democratic Movement (ODM) mwaka 2007.

Uchaguzi wa mwaka huo ulikumbwa na utata na baada ya serikali ya muungano kati ya Bw Odinga na Rais Mwai Kibaki kuundwa, ambapo Bw Odinga aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu, Bw Miguna alihudumu kama mmoja wa washauri wake kati ya 2009 na 2011

Wawili hao walizozana na Bw Miguna akawa mmoja wa wakosoaji wakuu wa Bw Odinga.

Aliandika kitabu kwa jina Peeling Back the Mask ambapo alimkosoa sana Bw Odinga na uongozi wake.

Mwaka 2013, alimuunga mkono Bw Kenyatta katika uchaguzi wa urais mwaka huo.

Lakini alibadilisha tena msimamo wake na kurejea upande wa Bw Odinga mwaka 2017, mwaka ambao aliwania pia wadhifa wa Gavana wa Nairobi katika uchaguzi uliofanyika Agosti ingawa kama mgombea ambaye hakuwa na chama.

Januari 30 mwaka huu, ndiye aliyetia saini hati ya kiapo cha Bw Odinga kuwa 'Rais wa Wananchi'.

Bw Odinga alipokutana na Bw Kenyatta mnamo 9 Machi na wakaahidi kuunganisha Kenya, Bw Miguna ni miongoni mwa waliomkosoa kiongozi huyo wa upinzani kwa hatua hiyo akisema huo ulikuwa sawa na usaliti.