Walichosema viongozi Afrika Mashariki kumhusu Winnie Mandela

Winnie Mandela, former wife of former South African President Nelson Mandela attends the opening of the 53rd National Conference of the African National Congress (ANC) on December 16, 2012 in Bloemfontein.

Chanzo cha picha, AFP

Mwanasiasa na mwanaharakati aliyepigana dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini Winnie Madikizela-Mandela alifariki dunia Jumatatu akiwa na miaka 81.

Alikuwa mke wa zamani wa rais wa kwanza mweusi Afrika Kusini Nelson Mandela.

Alikuwa nembo kuu ya vita dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi, na ingawa sifa zake ziliingia doa miaka ya baadaye, lakini bado alitambuliwa kama mtetezi wa wanyonge.

Winnie alifahamika sana na wengi kama Mama wa Taifa na viongozi wa nchi mbalimbali pamoja na wanasiasa wametuma salamu za rambirambi wakimkumbuka.

Hapa, tunaangazia baadhi ya ujumbe huo.

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Moussa Faki amesema Winnie Madikazela-Mandela "atakumbukwa daima kama mtu maarufu duniani, mtetezi wa haki asiye na woga aliyetoa kafara maisha yake kwa ajili ya uhuru Afrika Kusini na kwa wanawake kote."

Bi Gertrude Mongella, rais wa kwanza wa Bunge la Afrika ambaye pia ni mwanasiasa wa muda mrefu Tanzania amesema alikutana na Bi Mandela wakati wa harakati za mapambano, akizunguka dunia nzima ambapo alikuwa anatafuta kila njia kukabiliana na utawala wa ubaguzi wa rangi na kutetea kuachiliwa huru kwa Mzee Nelson Mandela na anamkumbuka sana kwa juhudi zake hizo.

Maelezo ya picha,

Bi Mongella alikutana na Bi Mandela mara nyingi

Rais wa tanzania John Magufuli ameeleza kusikitishwa kwake na kifo cha Bi Mandela na kusema "atakumbukwa kwa mchango wake katika kukabiliana na utawala wa ubaguzi wa rangi."

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alisema alipokea habari hizo za tanzia kwa "masikitiko" na kusema "tumempoteza shujaa na mkombozi".

"Katika maisha ya Winnie Madikizela-Mandela, aliyestahimili na kushinda, tunatazama waziwazi gharama ya uhuru."

"Ujasiri wake na utuhamasishe kuutumia vyema uhuru ambao alipigania na kutushindia."

Rais wa Uganda Yoweri Museveni pia alisema alisikitishwa sana na kifo cha Bi Mandela.

"Namheshimu kwa mchango wake katika juhudi za kupigania ukombozi wa Afrika Kusini, hasa wakati Mzee Mandela alipokuwa gerezani."

Kiongozi wa upinzani Tanzania Zitto Kabwe amemweleza Bi Mandela kama "Mwanamke aliyebeba bendera ya mapambano wakati wanaume wakiwa jela au uhamishoni."

"Hakika alichofanya wanaume wengi tungeshindwa. Nomzamo ni Mama wa Afrika," amesema.