Zitto: Nitampeleka Abdul Nondo Uhamiaji

Zitto Kabwe ni Mbunge wa Kiogma Mjini, Jimbo analotoka Abdul Nondo

Chanzo cha picha, Nondo Facebook/ Kabwe Twitter

Maelezo ya picha,

Zitto Kabwe ni Mbunge wa Kiogma Mjini, Jimbo analotoka Abdul Nondo

Mbunge wa Kigoma mjini Zitto Kabwe amesema atamsindikiza kiongozi wa mtandao wa wanafunzi Abdul Nondo katika makao makuu ya uhamiaji Tanzania.

Hii ni baada ya taarifa iliotoka kutoka mtandao huo ambao ulieleza kuwa Bw Nondo alipata barua ya kuitwa na uhamiaji ili 'akahojiwe kuhusu taarifa za uraia wake pamoja na za ndugu zake.'

Taarifa hizo zilisema 'afisa uhamiaji mkoa alitamka kuwa sheria inawaruhusu kumuhoji mtu yeyote wanaotilia mashaka uraia wake. Na kuwa wanamashaka na uraia wa Abdul Nondo,hivyo awathibitishie kuwa yeye ni Raia wa Tanzania.'

Abdul Nondo anashatakiwa kwa kosa la kudanganya kuwa alitekwa na kudaiwa kutoa taarifa za uongo mtandaoni.

Taarifa za kupotea kwa Bwana Nondo katika mazingira ya kutatanisha ziliibuka tarehe 6 Machi baada ya Nondo kutuma ujumbe kwa mmoja wa marafiki zake usiku wa manane akisema kuwa usalama wake uko hatarini.

Hali hiyo ilipeleka taharuki miongoni mwa wanafunzi wenzake na jamii kwa ujumla huku wengi wakidhani kuwa bwana Nondo alikuwa ametekwa.

Sasa Bw Nondo anatakiwa kurudi uhamiaji tarehe 20 mwezi Aprili na 'kupeleka cheti chake cha kuzaliwa, cheti cha kuzaliwa cha baba yake, mama yake, cha bibi na babu mzaa baba na mzaa mama.'