Tanzania imezindua chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi

Image caption Binti akionyesha kadi yake baada ya kupokea chanjo

Serikali ya Tanzania imezindua kampeni ya chanjo ya kuzuia saratani ya shingo ya kizazi.

Zaidi ya wasichana laki 6 walio na umri kati ya miaka 9 hadi 14 watachanjwa nchini nzima.

Image caption Duniani, kuna zaidi ya wanawake 260,000 wanaofariki kwa sababu ya saratani ya shingo ya kizazi

Huenda chanjo hii ikawakomboa wanawake na wasichana wengi kama wakijitokeza na kupata chanjo mapema zaidi.

"Saratani ya shingo ya kizazi ndio inayojitokeza zaidi Tanzania na ni chanzo cha vifo na magonjwa yanayohusiana na saratani miongoni mwa wanawake nchini."meneja wa mradi Daphrosa Lyimo aliiambia BBC.

Image caption Msichana mmoja akiandikishwa katika zoezi la uzinduzi

"Duniani, kuna zaidi ya wanawake 260,000 wanaofariki kwa sababu ya saratani hii, ambayo inazuilika na inatibiwa ikigunduliwa mapema." aliongezea Bwana Lyimo

Serikali ina matumaini kuwa kampeni hiyo itapunguza gharama za afya. Kumuuguza mgonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi kunaweza kugharimu takriban dola za Marekani elfu 2 wakati dola 15 zitatumika kuwachanja wasichana maafisa walisema.


Saratani ya shingo ya kizazi ni nini?

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Saratani ya shingo ya kizazi inzuilika na chanjo ya HPV

Saratani ya shingo ya kizazi ni saratani ambayo hutokea kwenye shingo ya kizazi cha mwanamke - ambayo ni kiingilio kutoka uke hadi katika mfuko wa uzazi.

Ni moja kati ya zaidi ya aina 100 ya virusi vya human papilloma (HPV), ambavyo 13 vinasababisha saratani.

Pia aina fulani ya HPV vinaambukizwa kwa njia ya ngono.

Baadhi ya sababu za kupata ugonjwa huo ni kushiriki ngono ukiwa na umri mdogo, ukifanya ngono na washiriki wengi , kuvuta sigara na kuwa na virusi vya Ukimwi.

Dalili ni

 • kupata hedhi kwa mzunguko usio wa kawaida au kutoka damu baada ya kujamiana
 • maumivu ya mgongo, mguu na fupanyonga
 • uchovu, kupungua kwa uzito na kutokuwa na hamu ya kula
 • maumivu kwenye uke au kutoa harufu mbaya
 • kuvimba kwa mguu mmoja

Uchunguzi wa virusi hivyo unastahili kufanyika ili kuvigundua mapema. Chanjo za HPV ni hatua nyingine ya kuziuzi.

Matibabu kwa wagonjwa walio na virusi hivyo yanategemea na viwango vya virusi hivyo mwilini, hata hivyo yanaweza hitaji kutibiwa kwa njia ya upasuaji na kutoa sehemu au mfuko wa uzazi mzima au kutumia miyonzi.

Chanzo: Shirika la Afya duniani


Mambo kumi unayoweza kufanya kupunguza hatari ya kuugua saratani:

 • Usivute sigara wala kutumia tumbaku ya aina yoyote
 • Hakikisha nyumbani kwako hamna moshi
 • Kula chakula chenye afya
 • Kunyonyesha kunapunguza hatari kwa mama kuugua saratani
 • Hakikisha watoto wako wanapata chanjo dhidi ya hepatatis B na HPV
 • Epuka kuchomwa sana na miale ya jua, au tumia mafuta yanayo kukinga dhidi ya miale hiyo.
 • Punguza uchafuzi wa hewa ndani na nje ya nyumba
 • Jishughulishe kuupa mwili mazoezi
 • Punguza unywaji wa pombe
 • Jitahidi kufanyiwa ukaguzi wa mapema kutambua uwepo wa saratani.

Mada zinazohusiana