Marekani inapima hatua za kujibu shambulio 'kemikali nchini Syria

Mtambo wa Marekani wa kuangamiza makombora USS Donald Cook, ukiwa ndani ya bahari ya Mediterranean Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mtambo wa Marekani wa kuangamiza makombora unaolindwa na kikosi cha majini USS Donald Cook, uko kwenye bahari ya Mediterranian

Marekani inasema kuwa "tayari ana maamuzi mengi'' za kujibu shambulio linaloshukiwa kuwa la kikemikali nchini Syria, huku viongozi wa magharibi wakiendelea kupima hatua za kijeshi.

Msemaji wa Ikulu ya White House Sarah Sanders amewaambia wandishi wa habari kuwa hakuna ushahidi wa mwisho uliokwisha chukuliwa juu ya mashambulio ya kijeshi.

Lakini amesema Marekani inaziwajibisha Urusi na Syria kwa tukio hilo.

Image caption Tayari rais Donald Trump ameionya Urusi "kuwa tayari" kwa mashambulio ya makombora nchini Syria

Baraza la Kitaifa la Usalama la Marekani litakutana Alhamisi, huku waziri mkuu wa Uingereza PM Theresa May akiitisha mkutano wa baraza la mawaziri kujadili tukio hilo la Syria.

Wanaharakati, wahudumu wa uokozi na madaktari wanasema makumi ya watu walikufa katika mji unaodhibitiwa na waasi wa Douma Jumamosi.

Lakini serikali ya Bashar al-Assad -ambayo inapata uungwaji mkono wa kijeshi kutoka Urusi- imekanusha kutekeleza shambulio hilo.

"Rais ana maamuzi mengi ya kujibu shambulio na mengine yanajadiliwa ," Alisema Bi Sanders wakati wa kikao na waandishi wa habari Jumatano .

"Bado hatujaainisha ni hatua gani hasa tunapanga kuchukua ,"aliongeza Bi Sanders.

Image caption Waziri Mkuu wa Uingereza Bi Theresa May(kushoto) na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwapamoja wameahidi kushirikiana na Marekani kujibu shambulio la'' kemikali'' la Syria

Kauli hizo zinaonekana kama kusisitizia onyo la awali lililotolewa na rais Donald Trump awali aliposema kuwa Urusi hainabudi "kuwa tayari" kwa mashambulio ya makombora nchini Syria.

" Jitayarishe Urusi, kwasababu watakuja, wazuri na wapya 'watanashati!'" Bwana Trump alisema katika ujumbe wake wa mapema asubuhi kwneye ukurasa wake wa Twitter jana Jumatano.

Pia alimuita kiongozi wa Syria "mnyama anayeua kwa gasi".

Marekani, Uingereza na Ufaransa wamekubaliana kushirikiana na wanaaminiwa kujiandaa kwa mashambulio ya kijeshi ili kujibu shambulio hilo linalodaiwa kuwa la kikemikali la mwishoni mwa juma.

Waziri wa ulinzi wa Marekani James Mattis anasema Marekani bado inatathmini shambulio la kemikali, lakini akaongeza kuwa jeshi liko tayari "kuchukua hatua za kijeshi ikiwa zitafaa kama rais alivyobainisha.''

Ikulu ya White House imesema kuwa rais hajaainisha ratiba ya hatua maalum zitakazochukuliwa.

Mtambo wa kuangamiza makombora unaolindwa na kikosi cha majini cha Marekani , USS Donald Cook, yuko katika bahari ya Mediterranean.

Image caption Picha ya video ambayo haijulikani ilichukuliwa na nani inaonyesha watoto walioshambuliwa wakipata matibabu

Ni kipi kilichotokea Jumamosi?

  • Shirika la matibabu la Marekani na Syria linasema kuwa watu zaidi ya 500 waliletwa kwenye kituo cha matibabu katika mji wa Douma, uliopo katika jimbo la mashariki la Ghouta , karibu na mji mkuu Damascus, wakiwa na dalili "zinazoonesha kuwa walishambuliwa na kemikali".
  • Shirika hilo linasema dalili walizaokuwa nazo ni pamoja na ugumu wa kupumua, ngozi ya samawati , kutokwa na povu mdomoni , kuungua kwa mboni na "walikuwa na harufu kama ya kemikali ya chlorine".
  • VIta vya Syria: Trump ailaani Syria kwa 'shambulio la kemikali' la Douma.
  • Vita vya Syria: 'muafaka umekubaliwa' kuwaondoa watu waliojeruhiwa kutoka Douma.
  • Idadi kamili ya vifo ya na ni nini hasa kilichotokea haviwezi kuthibitishwa kwasababu eneo hilo halina mawasiliano.
  • Makadirio ya idadi ya watu waliouawa katika shambulio linaloshukiwa kuwa la kemikali ni kuanzia watu 42 hadi zaidi 60, lakini makundi ya kitabibu yanasema idadi hiyo inaweza kuongezeka baada ya wahudumu wa uokoaji kuweza kufika kwenye sehemu za chini za majengo ambako mamia ya familia walikuwa wamekimbilia kuepuka mashambulio ya mabomu.

Muwakilishi wa Ufaransa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa alisema gesi ya sumu ilitumiwa kwa makusudi kwasababu inaweza kusambaa hadi sehemu za chini za majengo hadi.

Marekani ,ufaransa na Uingereza wameongoza kampeni ya kimataifa ya kulaani shambulio hilo linalodaiwa kuwa la kemikali, huku serikali ya Syria na waungaji mkono wao Urusi wakikana kuwajibika kwao kokote na tukio hilo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii