Kwanini baadhi ya mataifa ya Afrika yanaendelea kutekeleza hukumu ya kifo?

Zana za kutekeleza hukumu ya kifo kwa njia ya umeme/stima Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara zimetajwa kupiga hatua katika harakati za kupinga adhabu ya kifo

Shirika la kutetea haki za Binadamu ulimwenguni, Amnesty International limesema idadi ya watu waliohukumiwa adhabu ya kifo imepungua mwaka uliopita ukilinganisha na miezi kumi na mbili nyuma.

Katika ripoti yake mpya imesema karibu watu elfu moja, walinyongwa mwaka 2017, huku asilimia themanini na nne ya watu hao adhabu yake ikitekelezwa katika nchi za Iran, Saudi Arabia, Iraq na Pakistan.

Image caption Kunyongwa imekuwa ni moja ya mbinu zinazotumiwa barani Afrika katika kutekeleza hukumu ya kifo

Aidha nchi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara zimetajwa kupiga hatua katika harakati za kupinga adhabu ya kifo. Huku nchi 20 za Afrika zikifutilia mbali adhabu hiyo.

Mfano Guinea ilifuta adhabu ya kifo kwa uhalifu wowote ule na Kenya ikiwa na msimamo kuwa adhabu ya kifo si ya lazima, licha ya kwamba bado inayo hukumu hiyo.

Burkina Faso pia imesifiwa kwa muswada wake wa katiba ambao unahusisha kipengele cha kuondoa adhabu ya kifo, na sheria mpya ya Chad inaruhusu utekelezwaji wa hukumu hiyo pale mtuhumiwa atakapobainika kuwa na hatia ya ugaidi.

''Watu wengi wanaounga mkono adhabu ya kifo wanasema adhabu ya kifo ikiwepo itasaidia watu hawatatenda uhalifu, lakini utafiti uliofanyika duniani kote unaonyesha kuwa hilo halisaidii'', amesema Seif Magango afisa wa Amnesty International kanda ya Afrika Mashariki katika mahojiano na BBC.

''Tunaikemea adhabu ya kifo ambayo tunaiona ni ya kinyama, kwasababu katika nchi kama Marekani adhabu hizi zinapotekelezwa unapata kuwa uchunguzi wa vinasaba unapofanywa inakuja kugundulika kuwa wakati mwingine aliyehukumiwa si aliyefanya makosa'', amesema Bwana Magango.

Licha ya kwamba nchi 20 barani Afrika zimefuta hukumu ya kifo kwa makosa yote bado Somalia na Sudan Kusini zimesalia kuwa nchi pekee zinazoendeleza hukumu hiyo hadi mwaka jana ukilinganisha na mwaka 2016 ambapo nchi tano zilikuwa zinatekeleza hukumu hiyo.

Image caption Licha ya kwamba nchi 20 barani Afrika zimefuta hukumu ya kifo kwa makosa yote bado Somalia na Sudan Kusini zimesalia kuwa nchi pekee zinazoendeleza hukumu ya kifo

Taarifa kuhusu sababu ya kutekelezwa kwa hukumu ya kifo Somalia na Sudan kusini

Somalia:

  • Somalia inatambua sheria ya kiislamu (sharia) na mahakama za kiislamu ambazo zinaidhinisha njia nyingine za kifo.Mfano njia za zinazotumiwa kwa misingi ya dini zinazotumiwa kuwaadhibu washukiwa wa uhalifu,ni pamoja na kukatwa kichwa na kupigwa mawe.
  • Hukumu nyingi za kifo hutumiwa kiholela zaidi na makundi ya silaha kama njia ya kuwaadhibu wapinzani wao.
  • Hukumu ya kifo ilitekelezwa na mahakama ya kijeshi dhidi ya watu 12 waliofanya mashambulio mwaka 2017.
  • 11 kati hukumu hizo zilitekelezwa Mwezi Aprili 2017 , dadi hiyo ni ile iliyoripotiwa na vyombo vya habari.
  • Kwasababu ya usiri unaozingira hukumu hiyo kali, ni vigumu kuelewa wastani kamili wa idadi matukio ya adhabu ya kifo
  • Jimbo lililojitangazia uhuru wake la Somalia la Puntland lilitekeleza hukumu ya kifo kwa wafungwa 12 mwaka 2017.
  • Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa takriban hukumu za kifo 64 zilitolewa mwaka 2016 nchini Somalia.
  • Na nyingi kati yake zilitekelezwa katika jimbo la Puntland, kufuatia kiwango kikubwa cha maasi yaliyotekelezwa na Al-Shabab katika majimbo ya Puntland na Galmudug, ambapo mahakama ya kijeshi iliwahukumu watu 43 kifo kwa kushirikiana na Al-Shabab mwezi Juni, 12 miongoni mwa waliohukumiwa kifo ni watoto. Kulingana na ripoti ya Umoja wa Mataifa kuihusu Somalia.

Sudan:

  • Sheria ya Sudan Kusini ya mwaka 2008 ya uhalifu ya kabla ya uhuru wa taifa hilo bado inatekelezwa ikielezea kuwa hukumu ya kifo itatekelezwa kwa kunyongwa.
  • Hata hivyo hukumu hiyo imekuwa ikitekelezwa na serikali pamoja na makundi ya uasi dhidi ya wapinzani wao.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii