Mwanaharakati wa Rwanda awa mmoja kati ya wanawake 10 mashuhuri duniani

Mwanaharakati wa Rwanda Godelive Mukasarasi atangazwa kuwa miongoni mwa wanawake 10 mashuhuri duniani
Image caption Mwanaharakati wa Rwanda Godelive Mukasarasi atangazwa kuwa miongoni mwa wanawake 10 mashuhuri duniani

Mwanaharakati wa maswala ya wanawake nchini Rwanda Godelive Mukasarasi amewekwa kwenye orodha ya wanawake 10 mashuhuri duniani.

Tuzo aliyopewa na Marekani Bi Godelive Mukasarasi inatokana na juhudi za shirika aliloanzisha nchini Rwanda la SEVOTA kusaidia wakinamama walionusurika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.

Amewekwa kwenye orodha hiyo na nchi ya Marekani ambao hivi karibuni walitunukiwa tuzo ijulikanayo kwa jina''International women of Courage " kutokana na shughuli za shirika lake la SEVOTA ambalo husaidia wanawake waliobakwa wakati wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda pamoja na watoto waliozaliwa kutokana na kitendo hicho.

Shirika hilo limekuwa likisaidia wakinamama hao kujijenga kimaisha, kupokea yaliyowapata na kuwapa upendo watoto waliozaa kwa namna hiyo.

Image caption Shirika la SEVOTA linawapa wanawake matumaini ya kuendelea na maisha yao

Shirika hilo aliloanzisha limeweza kukusanya watu wasiopungua elfu 10 ambao ni wanawake wajane wa mauaji ya kimbari na watoto yatima.

Kadhalika tuzo aliyopewa ni baada ya kile kilichotajwa kuwa juhudi zake kupigania kosa la ubakaji kuwa miongoni mwa makosa ya uhalifu wa kivita.

Image caption Wanawake hao wanajifunza kukbali yaliyawatokea wakati wa vita vya kimbari

"Ni kweli kwamba mwaka 96 Rwanda ilipotunga sheria ya kuadhibu waliofanya mauaji ya kimbari,tulipaaza sauti wanaharakati wote wa akinamama pia kwa msaada wa wabunge wanawake wote walisimama kwa kauli moja kwamba waliofanya makosa ya ubakaji lazima wawekwe katika ngazi ya kwanza ya wauwaji wanaohukumiwa adhabu kali" alieleza Mukasarasi

Wakinamama hao husaidiwa kujikimu kimaisha wakifanya kazi katika mashirika mbali mbali, lakini kubwa zaidi ni ushauri nasaha wa jinsi ya kukabiliana na matatizo yaliyowapata wakati wa mauaji ya kimbari na kuwaonesha upendo watoto wao waliozaa wakati wa kubakwa.

Wengi wao ni wanavijiji wanaojishughulisha na kilimo.

Image caption Wanawake wakijishughulisha na kilimo ili kupata kipato

Mwandishi wa BBC Yves Bucyana, alizungumza na mama mmoja aliyekuwa akipalilia shamba lake la nyanya kusini mwa Rwanda.Yeye ni miongoni mwa wakinamama waliobakwa na ambao husaidiwa na shirika la SEVOTA.

"Mtoto wangu hivi sasa ana umri wa miaka 23 anasoma chuo kikuu. Kutokana na ushauri nasaha niliopewa nimeishapokea moyoni mwangu yaliyonifikia na kumkubali mwanangu pia.Haikuwa rahisi ilichukua muda,lakini mnamo miaka kama 5 iliyopita ndipo nilianza kufikiria kuwa mtoto hana hatia yoyote na anastahili kupendwa.Hivi sasa ni ndiye rafiki yangu tunapendana kama mama na mtoto.Lakini hakika mwanzo ilikuwa vigumu" alieleza mama huyo.

Bi Godelive Mukasarasi anasema pesa za tuzo aliyotunukiwa zitatumika kusaidia watoto ambao wamekosa ada ya masomo ,wengi wao wakiwa chuo kikuu.