Je mkutano kati ya Moi na Raila una athari zozote za kisiasa 2022?

Rais wa zamani nchini Kenya Daniel Moi na kiongozi wa upinzani Raila Odinga alipotembelewa na kiongozi huyo siku ya Alhamisi Haki miliki ya picha Raila Odinga
Image caption Rais wa zamani nchini Kenya Daniel Moi na kiongozi wa upinzani Raila Odinga alipotembelewa na kiongozi huyo siku ya Alhamisi

Ziara ya kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya Nasa, Raila Odinga nyumbani kwa rais wa zamani wa Kenya Daniel Moi imewawacha wengi vinywa wazi na kuzua mjadala kuhusu uchaguzi wa mwaka 2022 nchini humo.

Mkutano huo unajiri mwezi mmoja baada ya bwana Odinga na rais Uhuru Kenyatta kuahidi kufanya kazi pamoja kwa lengo la kuunganisha taifa na wanatarajiwa kuzindua mpango wao katika siku chache zijazo.

Wakati wa ziara hiyo ya siku ya Alhamisi bwana Odinga aliandamana na seneta wa Vihiga George Khaniri na mbunge wa Mvita Abdulswamad Sharrif Nassir.

Image caption Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga

Kiongozi huyo wa upinzani alikaribishwa Kabarak na seneta wa Baringo ambaye pia ni mwana wa Moi Gidion Moi na katibu mkuu wa chama cha KANU Nick Salat.

Hatahivyo hivyo ziara hiyo ilizua hisia kali katika mitandao ya kijamii nchini Kenya huku ikikashifiwa na kuungwa mkono na wengine.

Afya ya Moi

Taarifa iliotumwa katika vyombo vya habari na msaidizi wa Raila Odinga bwana Dennis Onyango ilisema kuwa kiongozi huyo wa upinzani alimtembelea kiongozi huyo wa zamani ili kumtakia afya njema baada ya kulazwa hospitalini nchini Israel kwa takriban mwezi mmoja.

Kulingana na taarifa hiyo Bwana Odinga na Moi walidaiwa kuzungumza hali ya kisiasa nchini katika mkutano uliochukua takriban saa moja.

Image caption Makamu wa rais nchini Kenya William Ruto anatarajiwa kumrithi rais Uhuru Kenyatta wakati wa uchaguzi wa mwaka 2022

Taarifa hiyo ilisema kuwa rais huyo wa zamani alikuwa buheri wa afya.

Inadaiwa kwamba viongozi hao wawili pia walifanya mazungumzo ya kina kuhusu uchaguzi wa 2022 ambao ulimhusisha seneta Moi, kulingana na duru.

Mwana huyo wa mzee Moi kwa sasa anakabiliana kisiasa na makamu wa rais William Ruto ili kudhibiti kura ya bonde la Ufa kabla ya uchaguzi wa 2022 huku wafuasi wa makamu huyo wa rais wakimuona seneta huyo kuwa muharibifu katika kinyang'anyiro hicho.

Na huku uvumi ukisambaa kwamba Bwana Odinga alikuwa Kabarak, viongozi kadhaa wanaomuunga mkono bwana Ruto walikashifu hatua hiyo wakidai kuwa mkutano huo ulilenga kumzuia makamu rais kumrithi rais Uhuru Kenyatta.

Odinga ambaye ni mwa wa makamu wa rais wa kwanza nchini Kenya Jaramogi Oginga Odinga alishindwa kwa mara ya nne katika kinyanganyiro cha kuwania urais cha mwaka uliopita.

Raila Odinga

Bwana Odinga ni mwanansiasa ambaye huzua hisia kali nchini Kenya- kwa kuwa yeye hupendwa na wengi na vilevile kuchukiwa na wengi.

Hakuna mwanasiasa anayezua hisia tofauti kama yeye nchini.

Kwa wafuasi wake ni mpiganiaji wa demokrasia aliyejitolea katika vita dhidi ya udikteta lakini wengine wanamuona kuwa mwanasiasa mwerevu anayejipigania maslahi yake, ambaye yuko tayari kufanya lolote lile ili avune mamlaka.

Aliahirisha harakati zake za kugombea urais 2002, na kumuunga mkono Mwai Kibaki ambaye alimuangusha Uhuru Kenyatta katika uchaguzi uliokifanya chama tawala cha KANU kupoteza mamlaka kwa mara ya kwanza tangu kenya ijipatie Uhuru 1963.

Image caption Ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya

Bwana Odinga na wafuasi wake wanaamini kwamba alipokonywa ushindi wake katika uchaguzi wa 2007 wakati alipogombea kupitia chama cha ODM dhidi ya Kibaki.

Ni Uchaguzi huo uliozua machafuko ya kikabila ambayo yaliosababisha mauaji ya watu 1,300 huku zaidi ya watu wengine 600,000 wakiwachwa bila makao.

Itakumbukwa kwamba Raila Odinga aliteswa na kuzuiwa katika mazingira mabaya baada ya mapinduzi ya mwaka 1982 ambayo hayakufanikiwa na utawala wa rais wa zamani Daniel Moi.

Lakini kama wanavyosema wanasiasa, siasa hazina uadui wa kudumu.

Mada zinazohusiana