Uganda kuwapokea wakimbizi kutoka Israel

Maandamano yamefanyika nchini Israel kupinga mpango wa kuwaondosha waafrika kuelekea nchini Uganda Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Maandamano yamefanyika nchini Israel kupinga mpango wa kuwaondosha waafrika kuelekea nchini Uganda

Serikali ya Uganda imetangaza kuwa imekubali kuwapokea wakimbizi 500 wa Eritrea na Sudan kutoka Israel.

Kumekuwa na mjadala nchini Israel kuhusu wahamiaji wa kiafrika na kama wanaweza kuondolewa kupelekwa barani Afrika.

Waziri kutoka Uganda anayeshughulikia maswala ya wakimbizi,Musa Ecweru ameviambia vyombo vya habari kuwa hilo lililkuwa ombi kutoka kwenye serikali ya Israel.

Amesema wakimbizi 500 wamekubali kuhamishiwa nchini Uganda.

Ecweru amesema zoezi hili linategemea pia utayari wa wakimbizi kuingia nchini Uganda.

Wale tu ambao wana hati za ukimbizi za nchini Israel watafikiriwa.

Watakapowasili, watapitia utaratibu wa kuhakikiwa kwa ajili ya kuwa na uhakika.

Wale watakaokuwa wametimiza masharti watachagua kuishi kwenye makazi ya wakimbizi au maeneo ya mjini.

Uganda imekuwa ikisifika ulimwenguni kwa kuweka milango wazi kwenye sera zake za wakimbizi, kwa sasa inahifadhi wakimbizi milioni 1.4 kutoka kwa nchi jirani na nje.

Wakimbizi wanaowatunza ni kutoka Kaskazini Mashariki , DRC na nchi hiyo tayari imepata changamoto ya rasilimali.

Mwanzoni mwa mwezi huu Serikali ya Israel ilibadili mawazo kuhusu makubaliano ambayo awali yalitiwa saini na shirika la wakimbizi duniani,ambapo ilikubali kutokuwaondoa wahamiaji wa kiafrika takriban 37,000 .