Diamond ahojiwa na Polisi kuhusu picha za mitandaoni

Diamond Platnumz Haki miliki ya picha Diamond
Image caption Diamond Platnumz

Mwanamziki maarufu wa Bongo fleva Nasibu Abdul Juma maarufu Diamond Platnumz amekuwa akihojiwa na Polisi kuhusu video iliyosambaa kwenye kurasa mbalimbali za mitandao ya kijamii ikimuonyesha akiwa kitandani akicheza na mzazi mwenzake Hamisa Mobetto pia na mwanamke mwingine ambaye hajajulikana,picha zinazoelezwa kuwa hazina maadili.

Waziri wa habari,sanaa na michezo Dokta Harrison Mwakyembe amewaambia wabunge ni matokeo ya sheria mpya za mitandao zilizopitishwa mapema mwezi uliopita.

Awali serikali ilitaja changamoto kubwa inayolikabili taifa ni athari ya utamaduni wa nje katika maadili, mila na desturi za Mtanzania kutokana na kuwepo na muingiliano mkubwa wa watu duniani.

''Kuna baadhi ya wasanii wetu ambao wamekuwa wakifanya uhuni uhuni ndani ya mitandao jana tumeweza kumkamata mwanamuziki nyota Diamond tumemfikisha polisi na anahojiwa kutokana na picha alizozungusha na vile vile Nandi naye imebidi apelekwe Polisi kuhojiwa tunaangalia namna ya kuwapeleka mahakamani.

"Nitoe wito kwa vijana mitandao sio kokoro la kupeleka uchafu, hii nchi ina utamaduni wake tunahitaji kuulinda''. amesema Mwakyembe

Nandi pia ni mwanamuziki nyota, ambaye picha yake ya video ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha akiwa na mwanamuziki wa kiume Billnas ambaye inadaiwa kuwa mpenzi wake akiwa kwenye nguo yake ya ndani sambamba na mwenza wake kitandani.

Sheria hizi mpya za mitandaoni zimetungwa kwa ajili ya kudhibiti matumizi ya mitandao hiyo, huku wakosoaji wakisema kuwa sheria hizi zipo kwa ajili ya kukandamiza uhuru wa kujieleza nchini Tanzania.

Sheria inasemaje?

Iwapo watafikishwa mahakamani, wawili hao wanaweza kushtakiwa chini ya kifungu Sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 ambayo inakataza kuweka kwenye mfumo wa kompyuta au taarifa nyingine yeyote kwenye mfumo wa mawasiliano.picha mbaya, kama vile picha chafu za ngono.

  • 14.-(1) Mtu hatachapisha au kusababisha kuchapishwa kwa kupitia katika mfumo wa kompyuta-

(a) Ponografia; au

(b) Ponografia yoyote iliyo ya kiasherati au chafu.

  • Mtu akatayekiuka kifungu kidogo cha (1) atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani, atawajibika, iwapo ni uchapishaji kuhusiana na-

(a) Ponografia, kulipa faini isiyopungua shilingi milioni ishirini au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miaka saba au vyote; au

(b) Ponografia iliyo ya kiasherati au chafu, kulipa faini isiyopungua shilingi milioni thelathini au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miaka kumi au vyote.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii