Kuna mipaka kati ya uhuru wa kujieleza na Maadili?

Watumiaji wa mitandao wamekuwa wakilaumiwa kukiuka maadili Haki miliki ya picha Google
Image caption Watumiaji wa mitandao wamekuwa wakilaumiwa kukiuka maadili

Mitandao ya kijamii ni majukwaa ya kutoa maoni. Jamii imekuwa ikitumia majukwaa hayo kujieleza kwa kutumia sanaa, kutoa hotuba, kutoa mawazo au maoni, kwa njia ya maandishi, picha au michoro.

Mitandao kama Facebook, Tweeter, Instagram, Snapchat, Jamii forum, Whatsapp na mingine mingi imetumika kwa muda mrefu kutimiza azma hiyo.

Hata hivyo watumiaji wamekuwa wakikosolewa kwa kiasi kikubwa kuhusu namna wanavyoitumia mitandao hiyo.

Ukuwaji wa matumizi ya mitandao ya kijamii miongoni mwa watanzania hasa vijana umeifanya serikali ya Tanzania kuweka Sheria ya Kukabiliana na uhalifu Mitandaoni mwaka 2015 ambayo tangu wakati huo imekuwa ikikosolewa kwa kuwaandama watumiaji wa kawaida wa mitandao hiyo.

Ukiukaji wa maadili

Wiki moja baada ya kampeni ya #ifikiewazazi kusambaa mitandaoni nchini Kenya, mamlaka ilianza kuwatafuta vijana waliokuwa wamepiga picha mbaya kwenye maeneo ya umma.

Vijana kadhaa walijikuta matatani baada ya kukamatwa wakipiga picha mbaya hadharani na baadhi yao wanashikiliwa katika kituo cha polisi Nairobi.

Ripoti zinaonyesha kuwa vijana walikua katika bustani ya Michuki jijini Nairobi wakipiga picha chafu, wakifanya vitendo vinavyoelezwa kuwa vya 'kihuni'.

Polisi wamekuta picha chafu na dawa za uzazi wa mpango kwa vijana hao wadogo.

''Walikuwa wakifanya vitendo ambavyo mtazamaji hawezi kuvivumilia. Tumewakamata wasichana wadogo na kijana mdogo wa kiume wote chini ya umri wa miaka 18, alisema mkuu wa polisi wa kituo hicho, Robinson Thuku.

Hashtag hiyo #ifikiewazazi - ilileta ghadhabu mitandaoni juma lililopita, na ililenga vijana hao ambao walikuwa wakipiga picha mbaya ili picha hizo ziwafikie wazazi.

Sheria ya Tanzania kudhibiti matumizi mabaya ya mitandao

Mwanamuziki maarufu wa Bongo fleva Nasibu Abdul Juma maarufu Diamond Platnumz amekuwa akihojiwa na Polisi kuhusu video iliyosambaa kwenye kurasa mbalimbali za mitandao ya kijamii ikimuonyesha akiwa kitandani akicheza na mzazi mwenzake Hamisa Mobetto pia na mwanamke mwingine ambaye hajajulikana,picha zinazoelezwa kuwa hazina maadili.

Waziri wa habari, sanaa na michezo Tanzania, Dkt Harrison Mwakyembe amewaambia wabunge ni matokeo ya sheria mpya za mitandao zilizopitishwa mapema mwezi uliopita.

Serikali ilitaja changamoto kubwa inayolikabili taifa ni athari ya utamaduni wa nje katika maadili, mila na desturi za Mtanzania kutokana na kuwepo na muingiliano mkubwa wa watu duniani.

''Kuna baadhi ya wasanii wetu ambao wamekuwa wakifanya uhuni uhuni ndani ya mitandao jana tumeweza kumkamata mwanamuziki nyota Diamond tumemfikisha polisi na anahojiwa kutokana na picha alizozungusha na vile vile Nandi naye imebidi apelekwe Polisi kuhojiwa tunaangalia namna ya kuwapeleka mahakamani.

"Nitoe wito kwa vijana mitandao sio kokoro la kupeleka uchafu, hii nchi ina utamaduni wake tunahitaji kuulinda'' amesema Mwakyembe.

Nandi pia ni mwanamuziki nyota, ambaye picha yake ya video ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonyesha akiwa na mwanamuziki wa kiume Billnas ambaye inadaiwa kuwa mpenzi wake akiwa kwenye nguo yake ya ndani sambamba na mwenza wake kitandani.

Sheria hizi mpya za mitandaoni zimetungwa kwa ajili ya kudhibiti matumizi ya mitandao hiyo, huku wakosoaji wakisema kuwa sheria hizi zipo kwa ajili ya kukandamiza uhuru wa kujieleza nchini Tanzania.

  • Mtu hatachapisha au kusababisha kuchapishwa kupitia katika mfumo wa kompyuta ponografia au ponografia yoyote iliyo ya kiasherati au chafu.
  • Mtu atakayekiuka kifungu kidogo cha (1)atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani, atawajibika.
  • Iwapo ni uchapishaji kuhusiana na ponografia, kulipa faini isiyopungua shilingi milioni ishirini au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miaka saba au vyote kwa pamoja; au
  • Ponografia iliyo ya kiasherati au chafu, kulipa faini isiyopungua shilingi milioni thelathini au kutumikia kifungo kwa kipindi kisichopungua miaka kumi au vyote kwa pamoja.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii