Je kuna nafasi ya kura ya maoni kubadili mfumo wa uongozi nchini Kenya

Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga walisalimiana mnamo Machi kiashiria cha kuafikiana kwao kisiasa

Kumekuwa na mgawanyiko wa hisia katika majukwaa mbali nchini kama vile kwenye mitandao ya kijamii na hata wachangiaji mada hiyo kwenye vyombo vya habari nchini Kenya kuhusu kuidhinishwa mageuzi ya katiba kutoa nafasi zaidi za uongozi nchini.

Wafuasi wa upinzani wakionekana kushinikiza wito wa kufanyika kura ya maoni nchini mahsusi kuikarabati katiba ili kuweza kutoa nafasi ya Uwaziri mkuu na manaibu wake, nafasi zitakazopewa vinara wa upinzani nchini.

Upande wa pili baadhi ya wafuasi wa serikali wanaonekana kupinga wito huo wa kufanyika kura ya maoni na badala yake usubiriwe uchaguzi mkuu nchini mwaka 2022.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption 'Baba neno lako ndio kauli ya mwisho' ni ujumbe wa wafuasi wa upinzani - NASA - nchini Kenya

Miongoni mwa sauti nzito zinazosikika kushinikiza mageuzi hayo ya sheria ni za muungano wa upinzani nchini NASA.

Baadhi ya wanasiasa katika chama hicho wamesikika hadharani wakitaka kura ya maoni iandaliwe nchini kuwajumuisha viongozi wao wakuu serikalini.

Maafikiano ya kisiasa:

Wito wa kutaka kura ya maoni umeongezeka hususan baada ya kilichokuja kutajwa kwa umaarufu nchini " the handshake" kusalimiana kwa mkono kwa kinara wa upinzani Raila Odinga na rais Uhuru Kenyatta.

Wawili hao walikutana mwezi uliopita mbele ya umma kuashiria kuafikiana kisiasa kati ya wapinzani hao.

Ni hatua iliyonuiwa kuleta amani na utulivu nchini baada ya uchaguzi wa mara mbili mwaka jana nchini uliokumbwa na mzozo na mfarakano.

Katika uchaguzi wa August 2017 ushindi haukuja kama ilivyotarajiwa, na upinzani ulisusia uchaguzi uliofuata wa marudio Oktoba kutokana na walichokitaja kuwa hakuna nafasi ya kufanyika uchaguzi wa kuaminika nchini bila ya mageuzi walioyaitisha katika mfumo mzima wa uchaguzi.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Serikali ya Uhuru Kenyatta kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 27 mwaka jana, haikuwa tayari kujadiliana kuhusu serikali ya 'nusu mkate'

Hata baada ya Uhuru Kenyatta kutangazwa mshindi wa uchaguzi huo wa marudio uhasama wa kisiasa uliendelea kuwepo Kenya hadi kukutana huko mwezi jana kwa uhuru Kenyatta na Raila Odinga kujaribu kuganga yajayo.

Kwa kauli yake mojawapo ya vinara wa upinzani - Gavana wa jimbo la Mombasa -Hassan Joho hivi maajuzi ameeleza kwamba ajenda kubwa iliyonayo upinzani nchini ni kutaka kujumuishwa ndani ya serikali, na kupambana na kutengwa kwa baadhi ya jamii nchini.

Joho ameongeza kwamba katiba ni ya wananchi, na ikifika wakati Wakenya wakitaka katiba ibadilishwe, itabadilishwa tu.

Kura ya maoni ina maana gani?

Kura ya maoni ni kama utafiti wa kuweza kubaini maoni hususani katika masuala ambayo yanagusa maslahi mapana ya umma .

Imezoeleka kwamba tafiti hizi zinafanywa katika uwanja wa siasa kwa kuangalia watu wana maoni gani au wana mtazamo gani pale ambapo kuna matukio .

Hakuna wakati maalum ambao kura ya maoni ndio inapaswa kufanyika ,ila kama kuna jambo ambalo linahitaji kufanyiwa uamuzi au uenda likagusa maslahi ya wengi hivyo viongozi au wananchi mara nyingine hushawishi ili kura ya maoni ifanyike.

Ndio maana mara nyingi utafiti wa aina hii au kura hizi za maoni zinafanywa wakati wa uchaguzi na unaweza kukuta eneo fulani miaka mingi inapita bila watu kupiga kura ya maoni.

Mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka nchini Tanzania,Saidi Msonga anaona kwamba yaweza kuwa ni mapema mno kwa taifa la Kenya kupiga kura ya maoni .

Uchaguzi bado uko mbali na bado kuna kipindi kirefu ambacho watu wanaweza kubadili mitazamo yao.

Msonga anadhani kwamba labda wameamua kupiga kura ya maoni kwa sasa kutokana na siasa za Kenya kwa sasa kuwa na mvutano mara kwa mara hivyo labda wanataka kupima joto la watu kwa kipindi walichopitia ambacho kilikuwa cha mvutano,hivyo labda viongozi wanataka kupata tathmini lakini kwa upande wa kupiga kura ya maoni kwa ajili ya matokeo yajayo,ni ngumu kupata majibu yenye uhalisia.

Uchaguzi mkuu 2017

Msimamo wa serikali kuelekea uchaguzi mkuu wa Octoba 27 mwaka jana ni kwamba haikuwa tayari kujadiliana kuhusu 'nusu mkate' - neno linalotumika kwa umaarufu kisiasa nchini kuashiria serikali ya muungano itakayohusisha ushirikiano na upinzani.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Kulikuwa na vituo zaidi ya 27,600 vya kupiga kura vilivyofunguliwa kwa kura hiyo ya maoni mnamo 2010

"Hatutokaa katika vyumba vya mikutano kujadiliana na kugawana uongozi serikali. Ni wakenya wali na haki kuamua ni nani atakayekuwa rais," alisema rais Uhuru Kenyatta.

Mara ya mwisho Kenya iliandaa kura ya maoni ilikuwa ni Agosti 4 2010.

Wapiga kura waliulizwa iwapo wanakubali pendekezo la katiba mpya, iliyopitishwa na bunge mnamo Aprili mosi 2010.

Katiba hiyo mpya ilionekana kama hatua kubwa katika kuepuka ghasia zilizoshuhudiwa nchini baada ya uchaguzi mkuu mnamo 2007.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii