Madonna ashindwa kuzuia barua za uhusiano wake na Tupac Shakur kupigwa mnada

Madonna Haki miliki ya picha Reuters

Msanii wa muziki wa pop Madonna amepoteza kesi ya kumzuia rafikiye wa zamani kutouza barua za kuvunjika kwa uhusiano wa kimapenzi kati yake na Tupac Shakur, ikiwemo kichana.

Jaji wa New York alitupilia mbali kesi ya Madonna dhidi ya Darlene Lutz akisema kuwa muda wa kuvipata vitu hivyo umekwisha.

Mojawapo ya vitu hivyo ni braua ya kuvunjika kwa uhusiano kati yake na msanii Tupac Shakur aliyefariki 1996 ambaye alikuwa na uhusiano wa kisiri na Madonna.

Mnada huo sasa utafanyika mwezi Julai, kulingana na mtandao wa Burudani TMZ.

Madonna alidai kwamba hakujua kwamba bi Lutz alikuwa akimiliki barua za Tupac alizoandika 1995 hadi aliposikia kuhusu mnada huo wa mtandaoni mwaka uliopita.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Madonna na Tupac walikuwa na uhusiano wa kisiri kwa muda usiojulikana

Katika barua hiyo iliojaa hisia, msanii huyo wa Rap alimwambia Madonna kwamba kuwa na uhusiano na mtu mweusi kutamsaidia katika kazi yake na kwamba sura yake itaharibika iwapo ataanza uhusiano na mtu mweupe.

Wapenzi hao walikuwa katika uhusiano wa kisiri ambao ni hivi majuzi ambapo Madonna alikubali kutangaza wazi.

Msanii huyo na bi Lutz walikosana mwaka 2003 na baada ya kumaliza mgogoro kuhusu mchoro mwaka uliokuja, Madonna alitia saini barua ya kujiondoa katika madai yoyote ya rafikiye wa zamani , jaji Gerald Lebovits alisema katika uamuzi wake siku ya Jumatatu.

Hivyobasi alielezea kwamba nyota huyo wa muziki wa Pop hawezi tena kumshtaki kutokana na vitu alivyovipiga mnada.

Madonna aliiambia mahakama mwaka uliopita wakati alipojaribu kuzuia mnada wa vitu hivyo kwamba umaarufu wake haumpatia uwezo wa kutaka kuhifadhi hati yake ya faragha ikiwemo vitu kama hivyo.

Mawakili wa bi Lutz wamemshutumu Madonna kwa kuwa na vita vya kibinafsi dhidi yake.