Mange Kimambi: Mwanaharakati mwiba kwa serikali ya Magufuli

Mange Kimambi Haki miliki ya picha Instagram/Mange Kimambi
Image caption Mange Kimambi

Ikiwa ni zaidi ya miaka miwili sasa tangu Rais John Magufuli wa Tanzania aingie madarakani, rais huyo ameonesha kutokusita kukabiliana na wapinzani wake, kuanzia wanasiasa na hata viongozi wa dini.

Rais Magufuli amedhibiti shughuli za kisiasa za wapinzani. Mikutano ya hadhara na maandamano ya kisiasa vyote vimezuiliwa, huku viongozi wote wa juu wa chama kikuu cha upinzani cha Chadema wakiwa wanakabiliwa na kesi mbalimbali mahakamani ikiwa ni pamoja na makosa ya kusababisha vurugu.

Serikali ya Rais Magufuli, ambaye ni muumini mzuri wa kanisa Katoliki, imetishia kuzifutia usajili asasi zote za kidini ambazo aidha zinajihusisha na siasa au kuzungumzia siasa katika mahubiri ya ibaada.

Lakini sasa rais huyo anakabiliana na upinzani mkubwa katika utawala wake kutoka kwa mwanaharakati wa kisiasa ambaye ushawishi wake bado unawashangaza wengi.

Mange Kimambi, mwanamitindo aliyebadilika kuwa mwanaharakati wa siasa, ndie muasisi wa maandamano yanayaopangwa nchi nzima kupinga kile anachokiita kuwa ni muendelezo wa ukiukwaji wa haki za binadamu na uminywaji wa haki za kiraia nchini Tanzania.

Marufuku za utawala wa Magufuli

  • Maandamano na mikutano ya Kisiasa
  • Usafirishwaji wa madini nje ya nchi
  • Waliopata mimba shuleni wasirejee shule
  • Usajili wa meli mpya
  • Safari za nje kwa watumishi wa umma

Ikiwa yatafanyika, maandamano hayo yatakuwa ya kwanza yanayolenga kupinga mwenendo wa serikali ya Rais Magufuli.

Mange, akiwa na wafuasi karibu milioni mbili kwenye ukurasa wake wa Instagram, ambaye miaka miwili iliyopita aliutumia ukurasa wake Instagram kumuunga mkono Rais Magufulu wakati wa kampeni za urais, leo hii anautumia ukurasa huo huo kuitisha maandamano makubwa ya kumpinga Magufuli na serikali yake.

Haki miliki ya picha Google Trends
Image caption Wengi wanaamini habari hizi ndizo ziliwavutia watu wengi kuanza kumfuata katika kurasa zake za mitandaoni.Picha hii inaonesha tathmini ya watu waliomtafuta Magufuli sambamba na Mange kwenye mtandao wa Google

Mange ni mama wa watoto watatu anayeishi nao Los Angeles, nchini Marekani. Harakati za mama huyo kumpinga Rais Magufuli zilianza kwenye mitandao ya kijamii takribani miezi sita tu baada ya rais huyo kupinga kuonyeshwa mubashara kwa shughuli za bunge kwasababu za kiuchumi.

Wafuasi wake, wengine wakiwa watumishi wa umma, wamekuwa wakimtumia taarifa mbali mbali zikiwemo zile zinazoaminika kuwa nyaraka nyeti za serikali, kufichua kile wasichokubaliana nacho juu ya mwenendo wa serikali. Wapo wengi pia ambao wamekuwa wakimtumia picha na taarifa kuonyesha hali duni ya huduma za kijamii katika maeneo yao.

Mange ni mmoja wa watu wa kwanza nchini Tanzania miaka ya mwanzo ya 2000, ambapo alitumia kurasa zake kuzungumzia maisha yake na marafiki zake pamoja na mitindo ya mavazi. Lakini Mange alizungumzia pia habari binafsi mbalimbali za watu maarufu waishio ndani na nje ya Tanzania, wakiwemo walimbwende, wanamuziki na waigizaji filamu.

Mange, ambaye aliwahi pia kuomba ridhaa ya uteuzi kutoka Chama Cha Mapinduzi kuwania nafasi ya ubunge jijini Dar es Salaam, amejikusanyia wakosoaji wengi kama ambavyo alivyo na mashabiki wengi.

Wakosoaji wake wengi wamekuwa wakipuuza harakati zake za kisiasa kwa kile wanachodai wanachodai kuwa wakati mwingine Mange amekuwa akitumia lugha isiyo na staha hasa anapomkosoa Rais Magufuli na viongozi wengine wa serikali.

Image caption Polisi wamekuwa wakitahadharisha juu ya maandamano mara kwa mara

Lakini kwa wanaomuunga mkono, ukurasa wa Instagram wa Mange umekuwa jukwaa lao la kupaza sauti kuhusu changamoto za huduma za kijamii na mwenendo wa hali ya kisiasa nchini Tanzania

Wakati ambapo shughuli za kisiasa za vyama vya upinzani zimedhibitiwa na watu kadhaa wamekamatwa na kushtakiwa kwa kuikosoa serikali kwa namna ambayo mamlaka haikupendezwa nayo, ukurasa wa Instagram wa Mange umefanyika sauti kuu kwa wakosoaji wengi wa serikali ya Rais Magufuli

Na inaonekana serikali imekuwa ikimtilia maanani

Viongozi weaandamizi mbali mbali wa serikali na vyombo vya ulinzi na usalama nchini vimejitokeza kuonya vikali juu ya maandamano ambayo Mange amekuwa akiyapanga kupitia ukurasa wake wa Instagram

Katika mkutano wa hadhara mwezi uliopita Rais Magufuli alionya kwamba watakao andamana watamtambua yeye ni nani

"Baadhi ya watu wameshindwa kujihusisha na siasa za kweli na wanataka kuwaona tu watu wakiandamana barabarani..waache waandamane na watanijua mimi ni nani" alisema Rais Magufuli

Wachambuzi wa maswala ya kisiasa wanasema muendelezo wa tahadhari kutoka viongozi mbali mbali wa serikali juu ya maandamano hayo, ulithibitisha ushawishi wa Mange nchini Tanzania na uwezekano wa kufanyika kwa maandamano hayo.

Hata hivyo vyombo vya habari vya ndani vimeonekana kujitenga na kuchapisha taarifa zinazomuhusu Mange na maandamano anayoyaandaa.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Utafiti wa Twaweza

Wakosoaji wa serikali na wanaharakati wa haki za binadamu wameendelea kuonya kwamba haki za kisiasa na uhuru vyombo vya habari na watu kujieleza vimeendelea kuminywa nchini Tanzania. Hata hivyo serikali imekuwa ikitupilia mbali madai haya.

Mara ya mwisho wafuasi wa upinzani walipoandamana mwezi Februari, makabiliano yao na polisi yalisababisha kifo cha mwanafunzi Akwilina Akwilline ambaye inaelezwa kuwa alipigwa risasi kwa bahati mbaya.

Ikiwa maandamano haya yatafanyika ama la, ni jambo ambalo wengi wanasubiri kuliona. Lakini muitikio wa serikali katika kuapa kudhibiti maandamano haya umetafsiriwa na wengi kuwa ni mafanikio ya ushawishi wa Mange kupitia ukarasa wake wa Instagram tu, jambo ambalo vyama vingi rasmi vya upinzani nchini Tanzania vimeshindwa kulifanya.

Mada zinazohusiana