Afisa wa polisi ashinda tuzo kwa kukataa hongo Nigeria

Julius Adewale Adedeji
Image caption Julius Adewale Adedeji

Julius Adewale Adedeji amekabidhiwa tuzo ya kuwa afisa wa polisi anayefanya kazi kwa bidii na ubalozi wa Marekani kwa kuhudumia jamii.

Anasimamia kitengo cha upelelzi katika jimbo la Ekiti. Sasa ni sawa kusema kuwa maafisa wa polisi wa Nigeria hawana maadili mema . Je Julius anahisi vipi kuchukuliwa kama mfano mzuri?.

Alisema kwamba anahisi vyema kwa kutambuliwa kwani hakujuwa kwamba alikuwa akichungzwa na kwamba ataendelea kufanya kazi kwa bidii zaidi.

Julius anasema kwamba alipokea nakala ya barua kutoka kwa ubalozi wa Marekani na alikuwa na wasiwasi kuhusu barua hiyo.

''Nilidhani kwamba kulikuwa na mtu ambaye alikuwa akinifanyia mzaha lakini nilipowaona wajumbe wa ubalozi wa Marekani niliitupia barua hiyo jicho la pili ili kuthibtisha''.

Image caption Julius Adewale Adedeji akipokea tuzo yake kutoka kwa ubalozi wa Marekani nchini humo

Afisa huyo anasema kwamba tuzo hiyo kwa mujibu wa ubalozi huo ililenga kuwaaibisha maafisa wa polisi ambao wamekuwa wakipokea hongo na kuwatuza wale ambao wamekuwa wakifanya kazi yao kwa bidii.

''Mara nyingi sana watu wamekuwa wakinijia na kuniambia kwamba ningependa kuchukua pesa ngapi, lakini mimi nimekuwa nikiwaambia sina haja ya pesa, mimi nafanya kazi yangu-nafanya kile ambacho ni sawa'',alisema Julius.

Anasema kwamba amewahi kuzungumza na baadhi ya maafisa wenzake ili kuwarai kuwacha kuchukua hongo, kuwa waaminifu na kufanya kazi kwa bidii na baadhi yao wamekubali wito wake.

''Katika sekta yangu nimefenya kazi na maafisa ambao wanafanya makosa na nimewaambia kwamba fanyeni la haki na mungu atawabariki'', aliongezea.