Kampeni za kura ya maoni inayokumbwa na mzozo Burundi zimeanza rasmi

Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza
Image caption Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza

Kampeni zimeanza rasmi nchini Burundi za kura ya maoni iliokumbwa na mzozo ambayo huenda ikampa fursa rais Pierre Nkuruzinza kuendelea kuhudumu kwa miaka 14 ya ziada.

Tayari kiongozi huyo amehudumu kwa miaka 13 kufikia sasa na wakosoaji wa kiongozi huyo wanasema hapaswi kugombea tena uongozi kwasababu ni kinyume cha sheria.

Dhamira ya kura hii ya maoni ni kuruhusu kuikarabati katiba ili kubadili kipengee cha mihula atakayohudumu rais, iwe miaka saba kila mmoja badala ya mitano hivi sasa.

Na iwapo mageuzi hayo yataidhinishwa, hatua hiyo itaanza kutekelezwa mwaka 2020 hivyo basi kumpa nafasi rais Nkuruzinza kuhudumu hadi mwaka 2034.

Maguezi hayo yanayopendekezwa pia yatatoa fursa ya kuidhinishwa wadhifa wa waziri mkuu na kupunguza idadi ya makamu wa rais kutoka wawili na kuwa mmoja.

Upinzani hatahivyo unasema mageuzi hayo ya katiba yanatishia makubaliano ya amani ya Arusha yaliosaidia kumaliza vita vya kiraia nchini kati ya mwaka 1993 - 2006 yaliosababisha vifo vya zaidi ya watu laki tatu.

Huwezi kusikiliza tena
Tanzania yatahadharisha wahalifu waliotoka Burundi

Vyama 26 vimeruhusiwa kukampeni katika kura ya maoni iliyopangwa kufanyika Mei 17, baadhi yao vikionekana kuegemea upande wa chama tawala nchini CNDD FDD.

Siku ya Jumanne, Marekani imeshutumu 'ghasia, unyanyasaji na kutishiwa' kwa watu Burundi wanaoonekana kuipinga kura hiyo ya maoni.

Katika taarifa yake, wizara ya mambo ya nje ya Marekani imeelezea wasiwasi wake kuhusu mpango huo uliotajwa 'kutokuwa na uwazi' katika kuibadili katiba ya nchi.

Imesema jitihada ya viongozi wa sasa kusalia madarakani zaidi ya muda wanaostahili kuhudumu, inadhalilisha taasisi za demokrasia.

Haki miliki ya picha AFP

Taifa hilo limeshuhudia ghasia za kisiasa tangu Pierre Nkurunziza alipowania muhula wa tatu mnamo 2015.

Lakini wafuasi wake wanahisi hatua hiyo ni ya sawa kwasababu alichaguliwa na bunge na sio wananchi mnamo 2005 - mtazamo uliodhinishwa pia na mahakama ya katiba nchini.

Mambo 5 kuhusu Nkuruzinza:

  • Nkurunziza, alifuzu katika masomo ya michezo, na aliifunza timu ya soka ya jeshi nchini Muzinga na klabu ya Union Sporting.
  • Alikuwa mwalimu na mhadhiri msaidizi katika chuo kikuu cha Burundi.
  • Mamake alikuwa Muanglikana na babake Mkatoliki, gavana wa zamani aliyeuawa katika mauaji aya kimbari ya Wahutu mnamo 1972.
  • Wakosoaji wake nkuruzinza wanamtuhumu kuwa dikteta asiyetaka kuachia ngazi.
  • Nkurunziza alinusurika katika jaribio la kuipindua serikali mnamo Mei 2015 wakati mkereketwa wake katika jeshi Godefroid Niyombare alipotaka kumpindua.
Image caption Pierre Nkuruzinza akiwasilisha stakabadhi zake kwa tume ya uchaguzi kuwania urais wa Burundi

Nkuruzinza aliapishwa mwezi Julai kwa muhula wa tatu, ambao wapinzani wake wanasema ni kinyume na katiba

Tangu wakati huo, visa vimekuwa vikiripotiwa vya mauaji ya wafuasi na wapinzani wa serikali.

Zaidi ya watu 1000 wameuawa na maelfu wengine wameitoroka nchini wakihofia usalama wao.

Usalama unaimarishwa pakubwa, na onyo kali limetolewa kwa vyama vya kisiasa vinvyowashauri wafuasi wao kususia kura hiyo ya maoni kuwa huenda wakapewa kifungo cha hadi miaka mitatu gerezani.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii