Kero la uhaba wa maji kwa wakaazi Nairobi licha ya mvua kubwa.

uhaba wa maji

Mji wa Nairobi umekumbwa na ukosefu mkubwa wa maji. Wakaazi wengi wa jiji hulazimika kununua maji kwa bei ghali kutoka kwa wachuuzi. Hali hii inaendelea licha ya mvua kubwa inayoendea kunyesha.

Katika eneo la Rongai nje kidogo ya mji mkuu Nairobi, mmoja wa wakaazi wa eneo hili anaeleza jinsi imekuwa vigumu kapata maji.

''Nimeishi mtaa huu tangu miaka ya 80 na mpaka sasa, hatujawahi kuona tatizo kubwa la maji kama hili. Shida ya maji ni kubwa kiasi kwamba kutoka mwezi Januari mwaka huu, hutajapata hata tone la maji kutoka kwenye mabomba ya kampuni ya Nairobi water. Sasa imetubidi kutegemea wauzaji wenye visima kutuletea maji.''

Image caption Bwawa la Ndakaini eneo la Murang'a katikati mwa Kenya

Bwawa la Ndakaini eneo la Murang'a katikati mwa Kenya lina ukubwa wa ekari 600.

Kiwango cha maji kimepunngua katika bwawa hili kufuatia msimu mrefu wa kiangazi katika miaka michache iliyopita na hata mvua kubwa inayoendela kunyesha nchini haijabadili hali kwenye bwawa na hili limewaacha wengi na maswali.

Mvua hiyo imewaacha karibu watu nusu milioni kupoteza makaazi yao nchini.

Licha ya hayo kampuni ya kusambaza maji mjini Nairobi inadai kuwa eneo la sehemu ya chemichemi ya Aberdare haina maji ya kutosha, Meneja wa Mawasiliano wa kampuni hiyo akidai imewabidi kuanzisha mradi wa ugavi wa maji kukithi mahitaji.

Image caption Chanzo cha maji kinachoelekea katika bwawa la Ndakaini

Mbaruku Vyakweli ni meneja wa mawasiliano, Nairobi Water, anasema, ''Kwa bahati mbaya viwango vya maji vimekuwa vikipungua.Vimekuwa vikipungua kwa mwaka mmoja sasa.

Tulibuni mpango wa ugavi wa maji. Mradi huo unahakikisha kuwa tunasambaza maji yaliyoko kwa wateja wetu wote kwa usawa jijini Nairobi. Hatujakuwa na mvua ya kutosha.''

Huwezi kusikiliza tena
Vikapu vinavyotumiwa kuchemsha maji na kupika Tanzania

Tunaamua kwenda juu zaidi mlimani ili kutafuta majibu. Bwawa la ndakaini hupokea maji kutoka mito mitatu ambayo chanzo chake ni milima Abadare .

Kiwango cha maji kimepungua. Kipimo kilichowekwa kando ya mto huu kikiashiria upungufu huo.

Lakini kilomita chache tu kutoka Ndakaine hali ni tofauti kabisa. Katika mto Chania ambao pia chanzo chake ni milima Abadare , maji yanatiririka kwa kasi na viwango kuongezeka maradufu.

Lakini Gavana wa County hii ya Murang'a hakubaliani na maelezo ya kampuni ya kusambaza maji ya Nairobi.

''Ukitazama mto wa Chania kwa mfano,ni ushahidi wa kutosha kuwa mvua inanyehsa katika chemichemi ya Abardare.Kwa hivyo ni wao watueleze nini kinaendelea.Je inawezekana kuwa kuna mtu ambaye hachungi bwawa inavyofaa na labda inavuja?Mimi si mtaalama but nashuku tu.'' anasema Gavana Mwangi Wairia.

Idara ya utabiri wa hali ya hewa imeiambia BBC kuwa japo chemichemi ya Abadare haijapokea viwango vya juu vya mvua ikilinganishwa na maeneo mengi ya nchi,maji yaliyopo yanatosha kuchangia maji katika bwawa. Katika mtandao wa twitter mjadala wa bwawa la Ndakaine umekuwa ukipamba moto. Baadhi ya Wakenya wakihoji nini kinaendelea na wengine wakishuku iwapo maji yanaelekezwa kwingine kwa matumizi ya kibinafsi.

Na huku uhaba wa maji katika bwawa la Ndakaine ukiendelea , serikali imewekeza dola milioni 86 katika mradi mwingine wa maji katika eneo hilohilo. Ukifahamika kama The northern water collector tunnel mradi huo unatarajiwa kuvuna maji Zaidi katika chemichemi ya Abadare ili kumudu mahitaji ya maji mjini Nairobi. Lakini sasa wengi wanahoji utekelezaji wa mradi huo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii