Uganda yapinga ofisi za Umoja wa mataifa kuhamishwa Nairobi kutoka Entebbe

Rais Yoweri Museveni nchini Uganda Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Yoweri Museveni anaarifiwa kumuandikia katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, barua kuelezea kutoridhia pendekezo hilo

Bunge la Uganda limepinga mpango wa Umoja wa mataifa wa kuondowa kituo chake cha kikanda Entebbe kukipeleka mjini Nairobi Kenya.

Spika wa bunge Bi Rebecca Kadaga ameteuwa kamati ya bunge ya maswala ya mambo ya nchi za nje pamoja na mbunge Theodore Sssekikubo kulifuatilia swala hilo.

Tayari inaaripotiwa kuwa Rais Yoweri Museveni amemuandikia katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres barua kuelezea kutoridhia na kupinga pendekezo hilo la kuondolewa kwa kituo hicho.

Zaidi ya wafanyakazi 420 wakiwemo 134 kutoka nje ya nchi na raia wa Uganda 285 na wafanyakazi wanane wa Umoja wa mataifa wa kujitolea watakosa kazi kama kituo hicho mjini Entebbe kitaondolewa na kupelekwa mjini Nairobi Kenya mwezi ujao.

Mpango wa kuhamisha kituo cha kikanda cha Umoja wa mataifa cha Entebbe ulipendekezwa na katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres kulingana na ripoti ya tarehe Mei mosi ya kamati ya ushauri wa utawala na maswali ya bajeti yaani ACABO.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres

Wabunge wa Uganda wapinga mpango huo.

Mbunge wa jimbo la Lwemiyaga Theodore Ssekibugo amesema kuwa kituo hicho kilikuwa kinaingiza dola million 11 kwa mwaka na amewaomba wabunge waunge mkono Uganda iendelea kuwa makao ya kituo hicho.

'Naona jinsi tunaweza kutatua hili swala muhimu, sababu Uganda inatowa mchango mkubwa kwa Afrika. Kuna kikosi kikubwa cha kulinda amani nchini Somalia, Sudan kusini, Jamuhuri ya Afrika ya kati na sehemu nyingine.

Uganda inaweza kunufaika kwa kituo hiki cha Umoja wa mataifa. Kenya tayari imeshanufaika, kuna mawakala wengi wa umoja wa mataifa nchini mwao, na sasa hii moja tuliyo nayo wanaichukua?' amesema Ssekibugo.

Spika wa bunge Rebecca Kadaga amesema Uganda imetowa mchango mkubwa kwa Jumuia ya Afrika mashariki kuliko taifa jingine hivyo kituo hicho kinasitahili kubaki nchini.

'Uganda nafikiri tumelipa kwa damu yetu, tumetowa damu yetu katika Bara la Afrika, kuliko taifa jingine katika bara hili la Afrika. Nafikiri tunastahili kuungwa mkono'.

Nairobi ndiyo mji uliopendekezwa katika ripoti hiyo kuwa makao ya kituo kipya cha Umoja wa mataifa Afrika huku miji mingine, Budapest nchini Hungary ikipendekezwa kwa ajili ya kituo cha Ulaya na mji wa Mexico kwa ajili ya Marekani.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii