Tanzania: Mbunge aliyefungwa jela kwa 'kumtusi' Magufuli aachiwa kwa msamaha wa rais

Bw Joseph Mbilinyi Haki miliki ya picha HISANI
Image caption Bw Joseph Mbilinyi (wa kwanza kushoto)

Wizara ya mambo ya ndani nchini Tanzania imesema mbunge wa Mbeya Mjini Joseph Osmund Mbilinyi, aliyefungwa jela baada ya kupatikana na kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli aliachiliwa huru kwa msamaha wa Rais.

Kamishna Jenerali wa Idara ya Magereza Juma Malewa amesema hakufai kuwa na utata kuhusu kuachiliwa huru kwa mbunge huyo.

Bw Mbilinyi, maarufu kama Sugu, alifungwa katika gereza la Ruanda, Mbeya mnamo 26 Februari baada ya kuhukumiwa kifungo cha miezi mitano na mahakama ya hakimu mkazi Mbeya.

"Mfungwa huyo kama wafungwa wengine mara baada ya kupokelewa gerezani alipata msamaha wa theluthi moja ya kifungo chake na hivyo alitakiwa kuachiliwa huru tarehe 5 Juni 2018," amesema Dkt Malewa.

Rais Magufuli mnamo 26 Aprili wakati wa maadhimisho ya Sikukuu ya Muungano alitoa msamaha wa robo moja kwa adhabu ya wafungwa waliokuwa na sifa za kunufaika na msamaha wa Rais kwa mujibu wa Ibara ya 45(1)d ya Katiba ya Tanzania.

Masharti ya msamaha huo ni kwamba lazima mfungwa awe ametumikia robo moja ya adhabu yake baada ya kuondolewa theluthi moja ya kifungo.

Idara ya magereza imesema chini ya utaratibu huo kuna wafungwa 3,319 waliofaidika na 585 kati yao waliachiliwa siku hiyo ya Sikukuu ya Muungano.

Kundi jingine la wafungwa 2,734 walipunguziwa robo ya adhabu.

"Walibakia gerezani kumalizia sehemu ya vifungo vyao na kuendelea kuachiliwa kadiri ya tarehe zao ambapo mfungwa aliyekuwa namba 219/2018 Joseph Osmund Mbilinyi maarufu Sugu ni miongoni mwa wafungwa walionufaika, na msamaha wa rais na ameachiliwa leo tarehe 10 Mei, 2018 badala ya 5 Juni 2018 kwa mujibu wa sheria," amesema Dkt Malewa.

"Hivyo basi mfungwa namba 219/2018 Joseph Osmund Mbilinyi alipata msamaha huo kutokana na mamlaka ya Rais kwa mujibu wa Katiba."

Kuachiwa 'kiholela'

Sugu, ambaye ni mbunge kwa tiketi ya chama cha upinzani Chadema, aliachiliwa huru pamoja na mwenzake Katibu wa Chadema Kanda ya nyanda za juu kusini, Emmanuel Masonga, ambaye walifungwa pamoja baada ya kupatikana na makosa sawa.

Walidaiwa kutenda kosa hilo katika mkutano wa hadhara walioufanya 30 Desemba mwaka jana eneo la Shule ya Msingi Mwenge jijini Mbeya.

Akizungumza baada ya kuachiwa huru, mbunge huyo ameishutumu serikali na kusema kwamba alifunhwa "kiholela", kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi.

"Sikutaka kuhoji sababu za kutolewa, jana niliambiwa jiandae kesho (leo) tutatoka, basi

nasi tukasema haina shida kwa sababu sikuwa na sababu ya kuwa ndani. Naamini sikutakiwa kuwa gerezani."