Mama anayenyonyesha mtoto aaibishwa katika mgahawa Nairobi

Kisa hicho kimesababisha hisia kali Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Kisa hicho kimesababisha hisia kali

Mama mmoja Mkenya amezungumza kuhusu vile alivyonyanyaswa na wahudumu wawili wa mgahawa mmoja nchini Kenya kwa kumnyonyesha mwanawe .

Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 26 ambaye alijitambulisha kama Betty Kim alikasirishwa sana na kisa hicho cha tarahe 7 mwezi Mei katika mgahawa wa OLive Restaurant katika kundi moja la mtandao wa Facebook.

Chapisho hilo lilisambaa kwa haraka huku akina mama wakijitokeza na kumtetea na hata wakaamua kupanga maandamano katika mgahawa huo.

Hatahivyo mgahawa huo umewataka wateja wake kuwa watulivu huku ikiendelea kutatua swala hilo.

Katika chapisho lililowekwa katika mtandao wa Facebook mgahawa huo umemtaka Kim kujiwasilisha ili kuchunguza chanzo cha kisa hicho .

Umesema kuwa uligundua kisa hicho kufuatia machapisho katika mitandao ya kijamii.

  • 'Siwezi kunyonyesha katika choo'

Bi Kim aliambia BBC kwamba alivamiwa na wahudumu wa mgahawa huo alipokuwa akimnyonyesha mwanawe wa mwaka mmoja.

''Niikuwa nikisubiri ombi langu la mchuzi wa nyama, kabeji na mukimo wakati muhudumu wa kike ambaye tayari alikuwa amechukua ombi langu la chakula hicho aliponiambia kutoendelea la sivyo nifiche nilichokuwa nikifanya''.

''Niilishangaa kwa sababu nilikuwa nimewahi kunyonyesha mwanangu katika migahawa mingine na siku hio kulikuwa kunanyesha hivyobasi sikuwa na mahala pengine pa kwenda''.

Bi Kim anasema kuwa mwanawe alikuwa amechoka hivyobasi akaendelea kumnyonyesha.

''Niliamua kuendelea kumnyonyesha mwanangu kabla ya muhudumu mwengine wa kike ambaye aliniletea chakula changu aliponiambia kwa upole kwa kile nilichokuwa nikifanya ilikuwa tabia ya aibu'', alisema.

''Nilimuuliza kwa upole ni wapi kwengine ambako ningemnyonyesha mwanangu na akanionyesha chooni. Wakati huo nilihisi madharau na nikasita kunyonyesha. Bi Kim sasa anatumai kwamba meneja wa mgahawa huo ataomba msamaha''.

Maandamano ya kumuunga mkono yameandaliwa Mei 15 na baadhi ya wanawake na akina mama wanaonyonyesha .

Kulingana na chapisho lililosambazwa katika mtandao wa Instagram na Facebook, wanawake hao wanatarajiwa kuandamana kutoka bustani ya Uhuru jijini Nairobi hadi bunge na baadaye kuvamia mgahawa huo wa OLive ambapo watanyonyesha wana wao.

Mada zinazohusiana